HEDHI: Wasichana waliotegemea mpango wa sodo shuleni Kaskazini Mashariki sasa wakosa bidhaa hizo muhimu
Na FARHIYA HUSSEIN
WASICHANA kutoka eneo la Kaskazini Mashariki ambao walikuwa wanafaidika na mradi wa sodo shuleni wameiomba serikali kuu na ile ya kaunti kuingilia kati na kuwasaidia.
Wanasema tangu kufungwa kwa shule wanakosa bidhaa hizo muhimu kwa sababu hawana uwezo wa kujinunulia.
Mmojawapo wa wanafunzi hao ambaye kwa sasa anaishi katika kambi ya wakimbizi – kambi ya IDP – Kaunti ya Garissa anasema yeye pamoja na wenzake wamekosa njia ya kujisitiri wakati wa hedhi na hawana budi kutumia vitambara vinavyopatikana kwa urahisi.
“Tunashukuru tumepokea chakula na baadhi ya vitu muhimu kama sabuni. Lakini tunakosa sodo ambazo ni muhimu kwetu,” akasema mwanafunzi huyo.
Anasema, maisha yake yameathiriwa sana kambini baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.
“Tunachukua kitambaa cha nguo kuukuu na kukata vipande na kutumia kama sodo,” akaeleza.
Naye msichana mwingine kutoka Wajir anasema sodo walizokuwa wakipewa kila mwezi shuleni ziliwafaidi lakini tangu kufungwa kwa shule kwa sababu ya janga la Covid-19, wanakosa bidhaa hizo muhimu.
“Ikiwa shule zitaendelea kufungwa, inamaanisha tutalazimika kutafuta njia mbadala kujikinga,” akasema.
Mwanafunzi huyo kutoka Wajir anaongezea kuwa mbali na sodo, walimu waliwapa mafunzo ya jinsi ya kujikinga na mimba za mapema na masuala mengine yanayowaathiri vijana.
Hali ni sawia katika vitongoji vya Mandera.
“Ni aibu kumwambia mwenzako akufundishe jinsi ya kutumia sodo. Naomba serikali kutuangalia na kutupa suluhisho wakati tunabaki majumbani mwetu. Ikiwa mimi binafsi ninakosa bidhaa hiyo muhimu, ” akasema mwanafunzi huyo wa kike ambaye ni mkazi wa Mandera.
Wizara ya Elimu kwa muda mrefu imekuwa ikiangazia suala la wasichana wengi kukosa kwenda shuleni wawapo katika hedhi kwa kukosa sodo.
Kwa sasa wasichana wengi waliokuwa wanategemea mgao wa sodo shuleni wanakosa namna ya kupata vitambaa hivyo spesheli kutokana na hali duni ya maisha.