Makala

KAMAU: Imani za kidini zisiwe kikwazo kwenye vita dhidi ya corona

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

HAPANA shaka yoyote kwamba dini huchangia pakubwa katika maisha ya mwanadamu hapa duniani.

Bila uwepo wa dini, pengine mwanadamu angekuwa kama ombwe tu bila mwelekeo wowote.

Hivyo, dini na mafundisho yake huwa kama dira na kurunzi kuu immulikao katika kila hatua ya maisha yake.

Na ingawa msingi wa dini umekuwa nguzo kuu ya mwanadamu tangu uumba wa dunia, wakati mwingine imetumiwa na watu walaghai kumpotosha, hasa kuhusu masuala yanayohusu sayansi na siasa.

Katika muktadha wa sayansi, miongoni mwa masuala tata ambayo yameshuhudia mgongano wa kimtazamo ni mafundisho ya baadhi ya madhehebu kuwa, mwanadamu hapaswi kwenda hospitalini kupata matibabu.

Ingawa ni suala ambalo linaonekana kuwa rahisi kwa baadhi ya watu, uzito wake ni mkubwa, kwani si mara moja tumeyaona madhehebu fulani yakieneza imani hizo. Na ikizingatiwa uzito ambao watu wengi, hasa katika nchi zenye ukuaji kadri wa kiuchumi huchukulia imani za kidini, kuna wale huamini kabisa kuwa kwenda hospitalini ni “ushetani.”

Wengi hukita imani zao kwenye “nguvu za maombi” kama chemichemi ya uponyaji wao.

Kama mwanadamu anayeamini katika uhuru wa kiimani, kamwe siwezi kupinga imani ya mtu binafsi hata kidogo.

Hata hivyo, tatizo langu limo kwa baadhi ya viongozi wa kidini ambao bado wanaeneza nadharia hizi miongoni mwa washirika hao, hasa wakati huu dunia nzima inakabiliana na janga la virusi vya corona.

Baadhi wamenukuliwa wakidai hata kuwa na uwezo wa kuponya virusi, hivyo washirika wao hawapaswi kwenda hospitalini wala kuzingatia kanuni ambazo zimetolewa na serikali kuzingatiwa ili kudhibiti maambukizi yake. Mkasa mkuu ni kuwa, baadhi yao wamefariki huku bado wakiendelea kushikilia imani hizo.

Mfano mzuri ni kifo cha Pasta Franklin Ndifor kutoka Cameroon aliyefariki Jumapili wiki iliyopita kutokana na corona, licha ya kudai kuwaponya walioambukizwa.

Hapa Kenya, baadhi ya madhehebu ambayo yamehusishwa na imani kama hizo ni ile ya Kavonokia, kutoka eneo la Mashariki, ambapo wafuasi wake wengi hawaamini katika kwenda hospitalini.

Bila shaka, lazima viongozi wa kidini wazinduke mara hii kwa kutupilia mbali baadhi ya imani ambazo huenda zikahatarisha maisha ya wafuasi wao, hasa ikiwa serikali itafungua upya maabadi.

Alipomuumba mwanadamu, Mungu alimpa uwezo mkubwa kiakili kuliko wanyama wengine ili kumwezesha kusuluhisha changamoto zinazomkumba.

Isingekuwa hivyo, basi mwanadamu angekuwa mbumbumbu kama wanyama wengine.

Ni kupitia uwezo wa kiakili aliopewa na Mungu, ambapo mwanadamu ameweza kubuni mfumo wa elimu unaomwezesha kuwatoa wataalamu wa hali ya juu kama vile madaktari, wanasayansi, wahandisi, marubani kati ya wengine.

Hivyo, washirika wa madhehebu hayo pia lazima wazinduke; kwa kufahamu kuwa miongoni mwa sababu ambazo husababisha baadhi ya maafa ni kutojali kwa mwanadamu mwenyewe, licha ya kufahamu ukweli.

Huu ni wakati mwafaka wa kutupilia mbali imani zitakazoathiri juhudi za kukabili virusi hivyo.

 

[email protected]