• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Klabu za La Liga zataka soka ya Uhispania irejelewe Juni 8 badala ya Juni 12

Klabu za La Liga zataka soka ya Uhispania irejelewe Juni 8 badala ya Juni 12

Na CHRIS ADUNGO

LIGI Kuu ya Uhispania (La Liga) itarejelewa mnamo Juni 8, 2020, na mechi zote kuchezewa ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki; haya ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez.

Awali, Javier Tebas ambaye ni Rais wa La Liga, alikuwa amependekeza kipute hicho kuanza upya mnamo Juni 12 japo ripoti zinaarifu kwamba vinara wa klabu zote 20 za ligi hiyo wameafikiana kuwa tarehe ya Juni 8 ndiyo bora zaidi.

Wachezaji wa klabu zote za La Liga walirejea kambini mwanzoni mwa wiki iliyopita na wamekuwa wakishiriki mazoezi ya pamoja katika vikundi vya watu 10.

“Uhispania imefanya yote ambayo ilistahili kufanya na kwa sasa umefikia wakati wa kuleta upya katika maisha ya kawaida ya watu. Huu ndio wakati mwafaka wa kuwakubalia watu waendelee na shughuli zao za kila siku na ilivyo, sina sababu ya kutoidhinisha michuano ya Ligi Kuu ya La Liga kurejelewa Juni 8,” akatanguliza Sanchez.

“Tujiandae kwa La Liga kuanza upya mnamo Juni 8. Ligi yetu ni miongoni mwa zile zinazojivunia ufuasi mkubwa zaidi duniani na hatusatahili kuwanyima mashabiki wetu uhondo huu katika ulingo wa soka,” akasema.

Mbali na La Liga, kipute kingine cha soka kinachotazamiwa kurejelewa nchini Uhispania ni Ligi ya Daraja la Kwanza (Segunda). Gozi kati ya Sevilla na Real Betis ndio utakaokuwa mchuano wa kwanza kusakatwa pindi kampeni za La Liga zitakapoanza upya.

“Tunafurahia sana maamuzi haya. Kufaulu kwa marejeo ya La Liga mnamo Juni 8 ni zao la juhudi kubwa na ushirikiano wa kiwango cha juu kati ya vinara wa klabu, wachezaji, makocha, maafisa wa serikali na maafisa wa afya,” akasema Tebas huku akisisitiza kwamba washikadau wote wametakiwa kuendelea kuzingatia kanuni zilizopo za afya ili kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya homa kali ya corona.

Soka ya Uhispania iliahirishwa mnamo Machi 12 kutokana na janga la corona zikiwa zimesalia mechi 11 zaidi kwa msimu huu kukamilika. Wanasoka wa ligi mbili za kiwango cha juu katika soka ya Uhispania walikubaliwa kurejea katika kambi zao za mazoezi mwanzoni mwa mwezi huu baada ya kufanyiwa vipimo vya afya ili kubainisha iwapo wana virusi vya corona au la.

Wachezaji watano ndio walioishia kupatikana na ugonjwa wa Covid-19.

Kufikia sasa, Barcelona wanaselelea kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 58, mbili zaidi kuliko watani wao wa tangu jadi, Real Madrid.

Kwingineko, Ligi Kuu ya Ureno (Primeira Liga) itarejelewa rasmi mnamo Juni 3 kwa mechi kati ya Portimonense na Gil Vicente kisha Famalicao na FC Porto ambao kwa sasa wanaongoza msimamo wa jedwali kwa alama moja zaidi kuliko Benfica. Hadi ligi hiyo ilipoahirishwa mwanzoni mwa Machi 2020, zilikuwa zimesalia michuano 10 pekee kwa muhula huu kutamatika.

You can share this post!

Mario Gotze kuagana rasmi na Dortmund mwishoni mwa msimu huu

Kampuni ya Wachina ya Sinohydro yawapa chakula wakazi wa...

adminleo