Mafunzo ya bure ya saikolojia kwa wachezaji wa raga wa Kenya wakati huu wa janga la Covid-19
Na GEOFFREY ANENE
WACHEZAJI wa raga wa Kenya wameanza Jumatatu kupokea ushauri wa kisaikolojia unaolenga kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kuchukulia afya ya kiakili kwa uzito mkubwa wakati huu mgumu wa janga la virusi vya corona.
Wanasaikolojia Rowena Tirop na Kanyali Ilako wameamua kutoa huduma hizo bila malipo “ili wachezaji na makocha waweze kuimarisha viwango vyao vya utendakazi na afya yao ya kiakili kwa jumla”.
“Ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona umesababisha mabadiliko makubwa katika maisha yetu.
Umesababisha tabia za wachezaji kukaa tu badala ya kutumia nguvu zao mazoezini ambapo wamezoea. Hii imechangia kuongezeka kwa magonjwa ya kiakili kama mtu kuwa na wasiwasi kila mara, kukosa utulivu, kukasirika ovyoovyo na kuwa na mabadiliko ya sununu,” anasema Tirop, ambaye ni mwanasaikolojia wa masuala ya michezo na mazoezi.
Tirop aliwahi kushiriki michezo ya uogeleaji, mpira wa magongo na soka katika shule ya upili. Alifanya kazi na Shirikisho la Raga ya taasisi za elimu ya juu jijini London nchini Uingereza.
Anasema kuwa janga la virusi vya corona limevuruga taaluma za wachezaji “jinsi na inavyokuwa wanapopata majeraha ama kustaafu”.
Limefanya wachezaji wapunguze kwa kiasi kikubwa sana mazoezi ambayo wamezoea kufanya wakiwa na makocha na timu zao, anasema Tirop.
Wanasaikolojia hao wanasema kuwa lengo la kuanzisha ushauri huo ni kufanya kazi na watu binafsi na makundi kubuni ratiba zitakazofaa mahitaji yao ya kiakili.
“Tunahudumia mtu mmoja mmoja kushughulikia mambo kadhaa ya kikazi kwa kufahamu kila mteja wetu ili kuelewa jinsi akili yao inachangia vizuri ama vibaya katika utendakazi wao,” Tirop ameambia Taifa Leo katika mahojiano.
Tirop anafanya kazi na Shirikisho la Raga Kenya (KRU).
Ilako pia aliwahi kuwa muogeleaji. Amefanya kazi na waogeleaji wa Olimpiki nchini Finland, klabu ya soka nchini Ugiriki na akademia ya Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF) jijini Nairobi.
Yeye pia ni mtaalamu kwenye Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki ya walemavu wa kutia katika makundi watu walio na ulemavu wa kiakili wa kufahamu masuala ya elimu.