Makala

AKILIMALI: Mpigapicha mahiri ambaye alianza kujikimu kwa kuuza juisi

May 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na FARHIYA HUSSEIN

LICHA ya kuacha shule akiwa kidato cha pili, Bw Mohammed Mbwana hii leo ni miongoni mwa wapigapicha tajika katika Kaunti ya Mombasa.

Mbwana alipokutana na Akilimali, alisimulia pandashuka za maisha yake.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 anasema kuwa hakudhani ipo siku talanta yake itakuwa njia ya yeye kujipatia kipato.

“Nyumbani kulikuwa na changamoto za kifedha na hatukuweza kulipiwa karo sote. Niliona ni afadhali nijitume na kuacha shule ili wenzangu wapate masomo,” akasema Mbwana.

Hatua yake ya kwanza kwa biashara ilikuwa kuuza sharubati na nguo.

“Nilianza kuuza sharubati ambapo glasi niliiuza kwa Sh10 na chupa moja kwa Sh20 na kila jioni angalau nilikuwa nikienda nyumbani na Sh400, ” akasema.

Anasema baadaye aliachana na biashara hiyo na kujihusisha na uuzaji wa nguo barabarani.

“Nilifikiria kuwa wale wanaouza nguo hutengeneza pesa nzuri na nikaanza kutanga na njia nikitafuta wateja,” akasema.

Haya yote aliyafanya ili mkono uende kinywani.

Aidha Mbwana alikuwa mchezaji wa mpira katika klabu za mitaani.

“Nilikuwa nikiuza nguo mchana na jioni nilikuwa naenda kucheza mpira. Soka ilikuwa kama dawa kwangu. Sikulipwa kucheza mpira,” anasema.

Hata hivyo, maisha yake yalichukua mkondo mpya baada ya kujeruhiwa.

Baada ya miaka kadhaa ya kukaa nyumbani, aliamua kujaribu kitu kipya; kuwa mpigapicha.

“Yote yalianza na marafiki zangu. Nilikuwa nikiwapiga picha kwa kutumia simu zao. Wakaanza kunishawishi niweze kuutumia ustadi huo kitaaluma zaidi,” anasimulia.

“Siku moja binamu yangu alifika kutoka nchini Canada na wakati alirudi kwenye uwanja wa ndege alisahau kamera yake nyumbani, mjomba wangu akaichukua na kuitunza,” akasema.

Wenzake wa timu yake walikuwa na mchezo wa mpira wa miguu uliodhaminiwa na SportPesa ambapo aliona fursa ya kuitumia ile kamera.

“Nilimuomba mjomba ile kamera na kuelekea uwanjani nikiwa sijui chochote. Ni rafiki yangu mmoja aliyenielekeza jinsi ya kuitumia,” akaeleza kijana huyu.

Anasema alipiga picha za kupendeza kwa miaka miwili kabla ya kuamua kuifanya iwe ndiyo kazi yake kutegemea.

Biashara yake ndogo inategemea upatikanaji wa wateja.

“Naweza kumaliza wiki bila mteja lakini wakati biashara ni nzuri ninapata Sh10,000 kwa wiki,” akasema Mbwana.

Anakiri bado hajafungua studio lakini amejifunza mengi na sasa ana vifaa vichache ikiwa ni pamoja na kamera mpya, tarakilishi na hata ‘kigoda’ cha kamera kukalia yaani tripod.

“Tangu nilipoanza kupiga picha kama biashara, nimeweza kupata zaidi ya Sh100,000,” anasema.

Anapendelea kupiga picha za mazingira na za mpira wa miguu kwa sababu “tunahitaji kuthamini uzuri wa maumbile na mpira wa miguu.”

“Ikiwa unalalamika kuhusu ukosefu wa ajira, unaweza kubaki hivyo kwa muda mrefu. Ni vizuri ufikirie kuhusu talanta na ubadilishe kuwa ujuzi wa biashara,” anashauri.