Cherargei asema si neno kuondolewa katika kamati ya sheria seneti
Na SAMMY WAWERU
SENETA wa Kaunti ya Nandi Samson Cherargei amesema kupokonywa wadhifa wa Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Sheria si neno na kwamba sasa ataweza kuhudumia kikamilifu waliomchagua.
Bw Cherargei amesema hajalishwi na hatua hiyo iliyotajwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju kama ya kuleta nidhamu chamani.
Mabadiliko hayo ya kamati mbalimbali seneti Jumanne, yaliyotangazwa na kiranja seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, pia yaliathiri maseneta John Kinyua (Laikipia) aliyetimuliwa kutoka Uenyekiti wa Kamati ya Ugatuzi, Langat Christopher Andrew (Bomet) aliyepokonywa cheo cha Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, miongoni mwa wengine.
“Sijalishwi kuondolewa kama mwenyekiti wa kamati ya sheria, maisha lazima yaendelee. Hatua hiyo imeniondolea mzigo na sasa nitaweza kuhudumia wakazi wa Nandi kikamilifu,” seneta Cherargei akasema.
Akionekana kughadhabishwa na mabadiliko hayo, aliyoyataja yamechochewa kisiasa, Bw Cherargei alisema chama cha Jubilee kinapaswa kuonyesha ukomavu wa demokrasia kwa kufuata sheria.
Seneta huyo aidha alisema kung’atuliwa kwake si kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi ila ni kwa ajili ya siasa potovu chamani, zinazolenga kuzima ndoto za Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022.
Akifufua makovu ya kutimuliwa kwa seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) kama kiongozi wa wengi seneti, Prof Kithure Kindiki (Tharaka Nithi) naibu kiongozi wa wengi na Susan Kihika wa Nakuru kama kiranja, Bw Cherargei alisema ni bayana vita vya kisiasa vimeelekezwa kwa Dkt Ruto kupitia wandani wake.
“Ndio sasa milango ya kujitolea kwa sababu ya naibu rais imefunguliwa. Wengi wetu tutapitia tuliyoshuhudia,” Bw Cherargei akaeleza.
Alisema hayo Jumanne jioni kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.
Seneta huyo akieleza kushangazwa kwake na mkondo uliochukuliwa na chama tawala cha Jubilee, alisema matukio yanayoendelea kushuhudiwa ni ishara ya kukandamiza demokrasia chamani ikizingatiwa ni chama cha kitaifa.