RB Leipzig wapoteza fursa ya kupaa hadi nafasi ya pili kwenye jedwali la Bundesliga
Na CHRIS ADUNGO
RB LEIPZIG walipoteza fursa ya kupaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya utepetevu wao kuwaruhusu Hertha Berlin kutoka nyuma mwishoni mwa kipindi cha pili kulazimisha sare ya 2-2.
Hertha waliokuwa ugenini ndio waliotangulia kuona lango la Leipzig kupitia kwa Marko Grujic anayewachezea kwa mkopo kutoka Liverpool.
Bao hilo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Marvin Plattenhardt.
Hata hivyo, Leipzig walirejea mchezoni haraka na kusawazishiwa na Lukas Klostermann kunako dakika ya 24 kabla ya kusalia wachezaji 10 uwanjani baada ya Marcel Halstenberg kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 63.
Japo Patrick Schick aliwafungia Leipzig bao la pili katika dakika ya 68, Hertha walichuma nafuu kutokana na ukubwa wa idadi yao uwanjani na wakasawazishia mambo kupitia penalti ya Krzysztof Piatek kunako dakika ya 82.
Penalti hiyo iliyowanyima Leipzig alama tatu muhimu katika mchuano huo, ilitokana na tukio la fowadi wa zamani wa Everton Ademola Lookman kumchezea visivyo Matheus Cunha.
Leipzig walijibwaga ugani wakihitaji angalau alama tatu ili kuwapiku Borussia Dortmund katika nafasi ya pili kwa wingi wa mabao.
Sare waliyolazimishiwa kwa sasa unawasaza katika nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 55, tisa zaidi nyuma ya viongozi Bayern Munich wanaoselelea kileleni baada ya kuwapiga Dortmund 1-0 katika gozi lililosakatiwa ugani Signal Iduna Park mnamo Jumanne ya Mei 26.
Ushindi huo wa Bayern uliwaweka pazuri zaidi kutia kapuni ubingwa wa Bundesliga kwa msimu wa nane mfululizo.
Ni pengo la pointi mbili ndilo linalotamalaki kati ya Leipzig na Borussia Monchengladbach wanaofunga mduara wa nne-bora kwa idadi sawa ya alama na Bayer Leverkusen waliopepetwa 4-1 na Wolfsburg.
Zikiwa zimesalia raundi sita pekee kwa kipute cha Bundesliga kutamatika rasmi muhula huu, matokeo dhidi Hertha yanadidimiza kabisa matumaini finyu ya Leipzig kutawazwa wafalme wa soka ya Ujerumani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 11 ya kuwepo kwao.
Kabla ya hata kipenga cha kuashiria mwanzo wa mchuano huo kuanza, Leipzig walipata pigo la kujeruhiwa kwa kiungo mzawa wa Slovenia, Kevin Kampl wakati akipiga njaramba nje ya uwanja.
Kikosi hicho ambacho pia kinafukuzia ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, hakijawahi kumaliza kampeni za Bundesliga nje ya mduara wa sita-bora jedwalini katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita.
Leipzig kwa sasa wamo ndani ya robo-fainali za UEFA baada ya kuwapokeza Tottenham Hotspur ya Uingereza kichapo cha jumla ya mabao 4-0 katika hatua ya 16-bora.
Nambari bora zaidi ambayo Leipzig wamewahi kushikilia katika historia yao kwenye Bundesliga ni nafasi ya pili waliyoikamata mnamo 2016-17 chini ya kocha wa sasa wa Southampton, Ralph Hasenhuttl. Msimu huo, Bayern waliotawazwa mabingwa, walidumisha pengo la alama 15 kati yao na Leipzig.
Hertha ambao walichupa hadi nafasi ya 10 jedwalini kwa sasa wanajiandaa kuwaalika Augsburg mnamo Jumamosi kabla ya Leipzig kuwaendea Cologne mnamo Jumatatu ya Juni 1, 2020.
MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumatano):
Leipzig 2-2 Hertha Berlin
Union Berlin 1-1 Mainz
Augsburg 0-0 Paderborn
Dusseldorf 2-1 Schalke
Hoffenheim 3-1 Koln