• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
RIZIKI: Kwa zaidi ya miaka 20 anategemea uchomeleaji wa bidhaa za vyuma

RIZIKI: Kwa zaidi ya miaka 20 anategemea uchomeleaji wa bidhaa za vyuma

Na GEOFFREY ANENE

MIAKA 23 iliyopita, Willis Obonyo alichoka kuajiriwa na akatumia ujuzi aliopata kutoka kampuni kadhaa kujitosa katika biashara ya kuchomelea bidhaa za vyuma mtaani Kariobangi South Civil Servants jijini Nairobi.

Alipowasili katika eneo hili linalopakana na mtaa wa Dandora kwenye mkabala wa stegi ya matatu ya Wamwaris mwaka 1997, Obonyo anasema, alianza kwanza na kuchomelea madirisha na milango. Aligundua kuwa biashara hiyo ilikuwa inaweza kujisimamia.

“Nilianza pekee yangu, lakini baada ya muda, niliajiri mtu mmoja kwa sababu kazi iliongezeka. Kadri biashara ilivyoendelea kuwa kubwa baada ya kuongeza uchomeleaji wa viti na vitanda, ndivyo nilizidi kuongeza wafanyakazi. Biashara hii imeendelea kukuwa. Imekuwa ikiniletea faida,” anasema Obonyo.

Hata hivyo, baba huyo wa watoto watano anasema mkurupuko wa virusi hatari vya corona, ambavyo vinahangaisha dunia nzima, vimeathiri biashara yake baada ya kuthibitishwa kuingia nchini Kenya mnamo Machi 13.

“Virusi hivyo vilianzia nchini Uchina. Vyuma vingi, ambavyo tunatumia katika biashara hii vinatolewa Uchina… Tunaenda kwa maduka ya kuuza vyuma jinsi tumekuwa tukifanya, tunaambiwa kuwa Uchina kumefungwa na hakuna vyuma vinatoka huko. Tunaelezwa kuwa vyuma hivyo sasa vinatengenezwa hapa nchini. Biashara nyingi zinazojishughulisha na kutengeneza vyuma hapa Kenya zimefungwa kwa sababu serikali ilipiga marufuku mikusanyiko ya watu. Huwa zinakuwa na wafanyakazi wengi,” alieleza Taifa Leo.

Obonyo anasema kuwa malighafi yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye maduka sasa yamepanda bei.

“Kuna changamoto kwa sababu tulikuwa tumepanga na wateja waliokuwa wameweka oda kabla ya janga hili kufika Kenya. Hatuwezi kuwageuka. Tutamaliza kuunda bidhaa zao na kukubali kuwauzia kwa bei tuliyosikizana. Hii inamaanisha kuwa faida, ambayo tulitarajia kupata imeliwa na hali iliyoletwa na janga la corona baada ya bei ya vyuma kupanda,” anasema kabla ya kufichua pia kuwa janga hilo limechangia katika kutumia wafanyakazi wachache kwa sababu kila mmoja lazima akae mbali na mwenzake.

“Watu pia hawakuwa wamezoea kuvalia barakoa kwa hivyo mara kadhaa nimelazimika kurudisha mfanyakazi nyumbani ili aje akiwa ametii maagizo hayo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona. Hata hivyo, tatizo kubwa tunapata ni malighafi kupanda bei. Chuma cha futi 20 ambacho tulikuwa tunanunua sokoni kwa Sh400 sasa kimefika Sh520. Kuendesha kazi pia kumekuwa na changamoto zake kwa sababu ya mabadiliko sokoni. Unaenda katika duka la vyuma na unapata limefungwa ama unafika katika duka lililo wazi, lakini unapata bei inakaribia maradufu. Hata hivyo, tunajitahidi kutimiza mahitaji ya wateja kadri ya uwezo wetu,” anasema.

Obonyo anasema wakazi wa Kariobangi South Civil Servants wamechangia pakubwa katika ukuaji wa biashara yake ya kuchomelea vitanda.

“Biashara yangu ya vitanda ilianza kunoga wakati iliripotiwa kuwa kaunti ya Nairobi imevamiwa na kunguni karibu miaka miwili iliyopita. Wakazi wengi wa hapa waliamua kutupilia mbali vitanda vilivyotengenezwa kwa mbao kwa sababu kunguni mara nyingi hujificha katika mianya. Tangu wakati huo, watu wengi walianza kutumia vitanda vya chuma na kufanya biashara yangu kuimarika,” Obonyo anasema kabla ya kufichua kuwa zamani biashara ya kuchomelea vitanda ilikuwa ikifanywa na Wahindi na shirika la Huduma kwa Taifa (NYS) na jeshi. “Hao ndio watu walikuwa na ujuzi wa kuunda vitanda hivi, lakini kwa sasa uchomoleaji wa vitanda unafanywa hata watu wa mashinani kama sisi. Kutengeneza vitanda vya chuma kumefanya eneo hili kujulikana sana kiasi cha baadhi ya watu kuanza kuita stegi ya matatu ya Wamwaris kuwa steji ya vitanda kwa sababu wamekuwa wakiona hata malori makubwa yakija hapa na kujazwa vitanda vilivyonunuliwa. Nilianza na kitanda kimoja, lakini sasa natengeneza vingi,” anasema.

Taasisi kama shule, mahospitali na hata jeshi ni baadhi ya wateja wa Obonyo.

“Vitanda hivi unavyoona hapa ni vya jeshi la KDF. Pia, kuna taasisi nyinginezo zinazokuja hapa kutafuta vitanda. Vilevile, watu binafsi wanakuja kununua vitanda hapa.”

Aidha, Obonyo pia ameathirika na janga la corona kwa kushindwa kufika maeneo yaliyopigwa marufuku kama mtaa wa Eastleigh ama kuenda kaunti jirani kama Kiambu anapoitiwa kazi ya kupima madirisha, milango na vitanda, na kadhalika.

Mmojawapo wa wafanyakazi wa Willis Obonyo. Picha/ Geoffrey Anene

Obonyo alidokeza kuwa alipoanza kutengeneza vitanda ilimchukua siku mbili kukamilisha kitanda kimoja. Hata hivyo, baada ya kuajiri watu 15, sasa anachomelea vitanda 30 kwa siku moja. “Naamini kuwa fedha zaidi za kuwekeza zikipatikana, tunaweza kuchomelea vitanda 50 kwa siku. Changamoto inayotukumba mara nyingi huwa ni malighafi na fedha. Kama serikali inaweza kunisikiza, inafaa kutafuta mbinu za kusaidia sekta ya Juakali kwa sababu changamoto kubwa huwa ni kupata fedha za kuanzisha na pia kupanua biashara. Unaweza kupata malighafi leo na ikifika kesho ukose fedha za kuendesha biashara hiyo kwa sababu ya hasara fulani. Watu ambao tuko katika sekta ya Juakali tunafaa kusaidiwa na serikali na ninaamini tunaweza kuajiri watu wengi kuliko wale tuko nao tukipata usaidizi,” anasema.

“Kama Rais Uhuru Kenyatta ananisikiza sasa, ningependa kumuomba pia nifikiwe na fedha (Sh1.7 bilioni) ambazo serikali imetengea Wizara ya Afya kwa shughuli ya kutafuta vitanda kutoka kwa sekta ya Juakali kuongeza vitanda vya wagonjwa katika mahospitali ya umma. Hii ndio biashara tunafanya kila siku na ninaamini tunaweza kuchomelea vitanda. Tuko na wafanyakazi wanaoweza kufanya kazi hii. Watufikie sisi tuwatengenezee vitanda. Kama sasa kuna mambo haya ya kutenga wodi ama vituo vya wagonjwa wa Covid-19; tupewe hiyo kazi ya kutengeneza vitanda. Tunaweza kutengeneza vitanda vya ghorofa hata mbili. Tuko tayari kabisa kutengeneza vitanda hivyo na kwa haraka kwa sababu tutakuwa pia tumesaidiwa kuunda nafasi zaidi za kazi,” anasema Obonyo, ambaye hata hivyo, anahofia kuwa fedha hizo huenda zikaenda tu katika kampuni kubwa.

Anasihi Rais Kenyatta kupigania kuhakikisha kuwa fedha hizo zinafika watu wa juakali walio mashinani kama yeye.

“Naamini tukipata fedha hizo tutapiga hatua kubwa mbele kama nchi kwa sababu pia tutaajiri watu zaidi,” akaongeza.

Obonyo anasema kuwa kupitia biashara hiyo ameweza kusomesha watoto wake.

“Kifunguamimba amemaliza kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya, mtoto wangu wa pili yuko Utalii College karibu amalize, siishi kichakani nyumbani kwa sababu kupitia biashara hii nimejenga nyumba nzuri na sikosi chakula. Pia, nimeanzisha shule ndogo.”

Baadhi ya changamoto anazopata katika biashara hii wakati hakuna janga kama corona, Obonyo anasema, ni kuwa wafanyakazi wote si waaminifu.

Pia, wakati mwingine anapokea bili ya stima ambayo iko juu sana.

“Miaka miwili iliyopita pia nilipoteza vifaa vyangu vyote wakati wezi walikuja hapa na kuviiba,” anasema Obonyo. Pia, anakiri kuwa stima ikipotea kwa muda mrefu humletea hasara kubwa.

You can share this post!

Brescia wajuta kumsajili Mario Balotelli

KIKOLEZO: Vijiskendo kawapa jukwaa kuu showbiz

adminleo