Kahata arejea kambini mwa Simba SC huku ligi kuu ya TZ ikirejelewa rasmi Juni 13
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO matata wa Harambee Stars, Francis Kahata aliwasili jijini Dar es Salaam, Tanzania kuungana na wanasoka wenzake wa kikosi cha Simba SC.
Anakuwa mchezaji wa pili wa kigeni baada ya Meddie Kagere wa Rwanda kurejea kambini mwa Simba kwa minajili ya kukamilisha kampeni zilizosalia katika soka ya Ligi Kuu ya Tanzania msimu huu.
Wachezaji wa Simba walianza upya mazoezi ya pamoja mapema wiki hii baada ya serikali kufichua mipango ya kurejelewa kwa Ligi Kuu mnamo Juni 13, 2020.
Kahata amesema barua kutoka kwa vinara wa Simba SC ndiyo iliyomwezesha kuvuka vizuizi vya maafisa wa usalama barabarani kabla ya kuingia Tanzania licha ya amri inayoharamisha safari za abiria kwenye mipaka ya Kenya na Tanzania.
Simba ambao wanaongoza kilele cha jedwali la Ligi Kuu ya Tanzania walikuwa wamesalia na jumla ya mechi 10 muhula huu kabla ya ligi kusimamishwa mnamo Aprili kutokana na janga la corona.
Kahata anatarajiwa kuwa nguzo muhimu kambini mwa Simba ambao wanawania jumla ya mataji mawili kwa mpigo katika kampeni za msimu huu.
Washikilizi hao wa taji la Ligi Kuu wamepangiwa kuvaana na mabingwa watetezi Azam FC katika dimba la robo-fainali kuwania ufalme wa Kombe la FA Shield Cup nchini Tanzania mnamo Juni 28, 2020 katika uwanja wa kitaifa wa Dar es Salaam.
Simba kwa sasa wanajivunia alama 71 kwenye msimamo wa jedwali baada ya kupiga jumla ya mechi 28.
Azam wanashikilia nafasi ya pili kwa pointi 54 huku Mbeya City, Alliance FC, Mbao na Singida FC wakining’inia padogo mkiani.