Rais adokeza kuhusu shule na makanisa kufunguliwa
Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta ameagiza Wizara ya Elimu na ile ya Usalama wa Ndani kuharakisha mwongozo na mikakati ya kufungua shule na maeneo ya ibada itakayohakikisha usalama wa wanafunzi walimu na waumini.
Alisema haya huku idadi ya walioambukizwa iliyotolewa jana ikiwa 59 huku watano wakifariki, Nairobi na Mombasa. Jumla ya maambukizi sasa yamefika 2021 na waliokufa ni 69.
Rais alisema kwamba wazazi hasa walio na wanafunzi wanaofanya mitihani mwaka huu wana wasiwasi kuhusu hatima ya watoto wao na mikakati inafaa kufanywa ili kufungua shule kwa utaratibu.
“Ninaagiza wizara ya Elimu kuharakisha na kukamilisha mashauriano yanayoendelea na washikadau yatakayofanikisha shule nchini kuanza kufunguliwa,” alisema.
Rais alisema mwongozo wa kufungua shule unafaa kushirikisha kanuni ambazo shule na taasisi za elimu zitazingatia ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
Mnamo Ijumaa, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alisema kufunguliwa kwa shule kutategemea viwango vya maambukizi ya virusi vya corona nchini. Akizungumza alipopokea ripoti ya wataalamu waliotathmini uwezekano wa shule kufunguliwa na mikakati ya kuwahakikishia wanafunzi usalama wao, Prof Magoha alisema hali ilivyo kwa sasa hairuhusu shule kufunguliwa. Kenya imeendelea kuripoti visa vingi vya maambukizi ya corona.
Agizo la Rais Kenyatta linaashiria kuwa huenda wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha nne wakaruhusiwa shuleni kuanzia Septemba vilivyopendekeza baadhi ya vyama vya walimu na baadhi ya wazazi.
Kwenye hotuba ya Madaraka Dei, Rais Kenyatta pia aliagiza wizara za Afya na Usalama wa Ndani kushauriana na viongozi wa kidini kubuni mwongozo wa kufungua maeneo ya ibada.
“Kwa kutambua kwamba Kenya ni nchi inayomcha Mungu, ninaagiza wizara ya Usalama na wizara ya Afya kuhakikisha mashauriano na viongozi wa kidini kwa lengo la kuweka utaratibu wa kufungua maeneo ya ibada,” Rais alisema.