Klabu za EPL zakubaliwa kushiriki mechi za kirafiki
Na CHRIS ADUNGO
KLABU za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zimepewa kibali cha kushiriki mechi za kirafiki, chini ya masharti makali, kabla ya kurejelewa kwa kivumbi hicho mnmao Juni 17, 2020.
Klabu zinazonogesha kampeni za EPL muhula huu ziliomba idhini ya kuvaana wao kwa wao katika hatua muhimu ya kujifua kwa marejeo ya soka ya Uingereza. Maombi hayo ya klabu zote 20 za EPL yalikubaliwa na maafisa wa serikali ya Uingereza baada ya kushauriana vilivyo na maafisa wa afya na wasimamizi wa vikosi husika.
Liverpool ambao ni viongozi wa jedwali la EPL waliandaa mechi ya kirafiki iliyoshuhudia wanasoka 11 wa kikosi cha kwanza wakivaana na wenzao wa kikosi cha akiba uwanjani Anfield mnamo Juni 1, 2020.
Kwa mujibu wa kanuni ambao klabu za EPL zimewekewa, mechi za kirafiki zinaweza tu kuchezewa ndani ya viwanja vyao vya nyumbani au sehemu za kujifanyia mazoezi kambini. Aidha, wanasoka wote watakaoshiriki michuano hiyo lazima wawe wamefanyiwa vipimo vya afya kuthibitisha kwamba hawana maambukizi ya virusi vya corona.
Miongoni mwa masharti mengine ni pamoja na:
- Klabu zote isipokuwa Newcastle United ambayo italegezewa kanuni iwapo italazimika kuchezea nje ya uga wa St James’ Park, kutosafiri mbali na uwanja wao wa nyumbani kwa zaidi ya kipindi cha dakika 90.
- Wachezaji wote kuwasili uwanjani wakitumia magari yao binafsi, na ikiwezekana wakiwa wamevalia jezi kabisa.
- Hakuna marefa watakaokubaliwa kudhibiti mechi hizo. Baadhi ya maafisa wa klabu husika zinazovaana watatwikwa majukumu ya kusimamia na kuendesha mechi.
- Viwanja vyote na sehemu za mazoezi kukaguliwa vilivyo ili kubaini uwezekano wa hatari ya maambukizi ya virusi vya corona kabla ya mechi kupigwa.
Kocha Jurgen Klopp wa Liverpool amefichua kwamba wachezaji wake wamekuwa wakijifanyia mazoezi ndani ya uwanja mtupu ili kuzoea mazingira ya aina hiyo kipute cha EPL kitakaporejelewa.
Hakuna klabu yoyote itakayoruhusiwa kuchezea mechi katika uwanja wake wa nyumbani pindi baada ya kampeni za msimu huu kuanza upya.