• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Rais wa Lyon ataka Ligue 1 iendelee

Rais wa Lyon ataka Ligue 1 iendelee

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa klabu ya Olympique Lyon, Jean-Michel Aulas, ametaka serikali na vinara wa soka ya Ufaransa kubatilisha maamuzi ya kufutilia mbali kampeni za msimu huu mapema na kuhakikisha kwamba vipute vya Ligue 1 na Ligue 2 vilivyotamatishwa awali kutokana na janga la corona vinarejelewa.

Mnamo Aprili 28, 2020, wasimamizi wa soka ya Ufaransa walitamatisha kampeni za ligi mbili kuu za kabumbu nchini Ufaransa katika hatua iliyoshuhudia Amiens na Toulouse wakishushwa ngazi kwenye Ligi Kuu (Ligue 1) na nafasi zao kutwaliwa na Lorient na Lens waliopandishwa daraja kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza (Ligue 2).

Katika barua yake kwa Waziri Mkuu na Waziri wa Michezo, Aulas alisema hatua ya kusitishwa kabisa kwa ligi za soka ya Ufaransa muhula huu itakuwa na madhara makubwa zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na kitamaduni nchini humo.

Hadi msimu huu ulipotamatishwa, Lyon walikuwa wakishikilia nafasi ya saba jedwalini na hivyo hawatakuwa sehemu ya klabu zitakazonogesha kampeni za soka ya bara Ulaya msimu ujao.

Ligue 1 ndiyo ligi ya pekee kati ya Ligi Kuu tano za bara Ulaya kutamatisha msimu wao. Ligi za Uhispania (La Liga), Italia (Serie A) na Uingereza (EPL) zinatarajiwa kurejelewa Juni 2020 majuma machache baada ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kuanza upya mnamo Mei 16.

Ligi nyinginezo ambazo zimetamatishwa kabisa katika soka ya bara Ula ni zile za Uholanzi na Ubelgiji.

“Bundesliga ilianza upya Mei 16, La Liga itarejelewa mnamo Juni 11 kwa gozi kati ya Real Betis na Sevilla. Wachezaji wa Ligi Kuu nchini Italia, Urusi na Ureno wameanza mazoezi makundini na Uingereza inajizatiti kuhakikisha kwamba EPL inarejelewa kufikia Juni 17,” akatanguliza Aulas.

“Mbona Ufaransa walikuwa wepesi wa kutamatisha kampeni za msimu wao na kujidunisha kiasi hicho? Itakuwa vyema kwa maamuzi ya awali kubatilishwa na soka ya Ligue 1 kuanza upya. Hatua hiyo itawapa PSG ambao ni wawakilishi wetu barani Ulaya nafasi maridhawa zaidi ya kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA),” akaongeza.

EPL itaanza upya Juni 17 kwa mechi mbili zitakazokutanisha Aston Villa na Sheffield United kisha Manchester City na Arsenal. Mechi hizo ni zile zilizokuwa zimesalia kwa vikosi hivyo kucheza ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo wapinzani wote wengine 16 walikuwa wamepiga hadi kipute hicho kiliposimamishwa kwa muda kutokana na janga la corona mwanzoni mwa Machi 2020. Mechi zote za raundi nzima ya 30 zimeratibiwa kusakatwa kati ya Ijumaa ya Juni 19 na Jumapili ya Juni 21, 2020.

Serikali ya Ufaransa inatarajiwa kulegeza baadhi ya kanuni mpya zilizowekwa katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona mnamo Juni 3, 2020.

“Mbona tusiwazie Juni 3 kuwa siku mwafaka zaidi kwa Serikali kuwapa vinara wa soka fursa ya kuanza mikakati ya kurejelea kampeni za Ligue 1 msimu huu na kuhakikisha kwamba kipute hicho kinasakatwa kati ya Julai na Agosti?” akauliza Aulas.

Olympique Lyon ni miongoni mwa klabu tatu zikiwemo Amiens na Toulouse kuanza mchakato wa kisheria wa kutafuta haki mahakamani dhidi ya “maonevu” baada ya kutamatishwa rasmi kwa kampeni za Ligue 1 msimu huu.

  • Tags

You can share this post!

Kizungumkuti cha wawakilishi wa EPL katika UEFA

Riadha za Dunia za Continental Tour kuitwa Kip Keino Classic

adminleo