• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Riadha za Dunia za Continental Tour kuitwa Kip Keino Classic

Riadha za Dunia za Continental Tour kuitwa Kip Keino Classic

Na CHRIS ADUNGO

DURU ya Nairobi ya Riadha za Dunia za Continental Tour sasa itaitwa “Kip Keino Classic”. Haya ni kwa mujibu wa waandalizi wa kivumbi hicho.

Shughuli za kufanikisha mbio hizo za siku moja mnamo Septemba 26 katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 30,000 walioketi, zinaendelea vyema.

Makala ya kwanza ya riadha hizo yalikuwa yafanyike jijini Nairobi mnamo Mei 2, 2020 ila yakaahirishwa kutokana na ugonjwa hatari wa Covid-19.

Kwa mujibu wa Barnaba Korir ambaye ni mkurugenzi wa mashindano hayo, Kamati Andalizi imekuwa ikishughulisha usiku na mchana kuhakikisha kwamba mipango yote inakuwa shwari kabla ya kivumbi hicho kutifuliwa.

Licha ya duru hiyo kuitwa Kip Keino Classic kwa heshima ya veterani Kipchoge Keino, kivumbi cha fani ya mbio za mita 10,000 wakati wa riadha hizo kitaitwa “Naftali Temu 10,000m Classic”.

Kipchoge alijizolea nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Olimpiki za 1968 nchini Mexico kabla ya kutwaa medali nyingine ya dhahabu katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Olimpiki za 1972 jijini Munich, Ujerumani.

Kwa upande wake, Temu alitwalia Kenya nishani ya kwanza na ya mwisho katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki mnamo 1968 nchini Mexico. Kipchoge, Temu na Amos Biwott (mita 3,000 kuruka viunzi na maji), ndio Wakenya wa kwanza kunyakua medali za dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki mnamo 1968 nchini Mexico.

“Kipchoge ndiye baba wa Riadha za Kenya na dunia nzima inamfahamu zaidi kuliko Mkenya yeyote mwingine katika ulingo wa riadha,” akasema Korir kwa kusisitiza kwamba kuita mbio za mita 10,000 ‘Naftali Temu’ kutachochea zaidi Wakenya kutamba katika fani hiyo wakati wa Olimpiki zijazo jijini Tokyo, Japan.

Mwingereza Mo Farah na Waethiopia ndio wamekuwa wakitawala mbio za mita 10,000 duniani kwa kipindi kirefu kilichopita.

Shirikisho la Riadha la Dunia (IAAF), jiji la Turku nchini Finland sasa litaandaa duru ya ufunguzi wa riadha hizo za Continental Tour mnamo Agosti 11, 2020.

“Mbio hizo ni heshima kubwa kwa Kipchoge –  mwanariadha nguli ambaye tayari ameridhia kustahiwa kwa kiasi hicho,” akaongeza Korir kwa kusisitiza kwamba tayari wameandaa nembo ya mbio hizo ambayo itafichuliwa hivi karibuni.

“Tumekuwa katika mawasiliano ya mara kwa mara kwa waandalizi wa riadha hizo za dunia ili kuhakikisha kwamba kila kitu kinashughulikiwa ipasavyo. Ingawa mataifa mengi yana kanuni mpya zinazodhibiti usafiri wa nje kutokana na janga la corona, ni matumaini yetu kwamba ukawaida wa mambo utakuwa umerejelewa kufikia Septemba,” akaongeza Korir.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Jackson Tuwei amesema watalazimika kufanyia kalenda ya msimu huu mabadiliko kadhaa muhimu ili kuwawezesha wanariadha kujiandaa ipasavyo kwa makala hayo ya Continental Tour ambayo ni ya daraja ya chini kuliko Diamond League.

Mbio za Diamond League huenda zikarejelewa Agosti 2020 kwa mujibu wa kalenda mpya iliyofupishwa zaidi na IAAF. Duru ya kwanza ya mbio hizo imeratibiwa kufanyika jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14.

“Ni masikitiko makubwa kwamba wanariadha wetu walikuwa wamejiandaa kwa mapambano mengi ambayo tayari yamefutiliwa mbali msimu huu. Hata hivyo, kwa sasa tunaandaa kalenda mpya itakayowapa wengi wao fursa ya kujizatiti vilivyo kwa makala yajayo ya Diamond League na Kip Keino Classic,” akasisitiza Tuwei.

  • Tags

You can share this post!

Rais wa Lyon ataka Ligue 1 iendelee

Bournemouth ilivyotikiswa na Covid-19

adminleo