Rware FC yaamini kuteleza sio kuanguka
Na JOHN KIMWERE
LICHA ya kutofanya vizuri kwenye michuano ya Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu huu klabu ya Rware FC inaamini kwamba kuteleza sio kuanguka.
Timu hiyo awali ikifahamika kama Vision FC iliyobuniwa miaka 20 iliyopita ni miongoni mwa vikosi 14 vilivyokuwa vikishiriki kinyang’anyiro hicho kabla ya kusitishwa kufuatia kuzuka kwa mlipuko wa virusi hatari vya Corona mwezi Machi.
”Mechi hizo zilipositishwa tulikuwa tumekaa vibaya katika jedwali ila tunaamini tulishindwa kufana kwa kutokuwa na uzoefu wa kushiriki mechi za kiwango hicho,” amesema kocha wake, Edwin Kanyonyi na kuongeza kuwa bado hawajapoteza tumaini la kupiga hatua katika ngarambe hiyo.
Aidha alidokeza kwamba wanapania kuingia sokoni kusaka huduma za wachana nyavu kadhaa wapya na wazoefu ili kuchochea wenzao na kuwaongeza nguvu kukabili makali ya wapinzani wao.
Anasema janga la Corona limewazuia kuendeleza mpango wao hasa zoezi la kutafuta wachezaji wapya tayari kwa shughuli za kipute hicho. Kocha huyo alisema wanahisi kampeni za kipute cha muhula huu zilishuhudia ushindani wa kufa mtu.
Rware FC ilipandishwa ngazi kushiriki kinyang’anyiro hicho baada ya kuibuka miongoni mwa nafasi tatu bora kwenye kwenye kampeni za migarazano ya Nairobi East Regional League (NERL) msimu uliyopita. Timu zingine zilizopandishwa ngazi ni Uprising FC na Mbotela Kamaliza FC. Rware FC ya mtaani Mukuru Njenga, Nairobi ambapo hufanyia mazoezi katika Uwanja wa Vision.
Naye naibu wa kocha, Willis Odhiambo anasema anakiri kuwa ukosefu wa ufadhili unakwamisha mpango wao kkushiriki kampeni za soka la kipute hicho.
”Tumetoa mwito kwa wahisani popote walipo wajitokeze na kuzipiga jeki klabu za wachezaji wanaoshiriki mechi za soka la mashinani hapa nchini,” alisema na kuongeza kwamba kushiriki michezo ni ajira kama zingine. Kampeni za kipute hicho zilisimamishwa baada ya mkurupuko huo huku zikiwa zimechezwa mechi 15.
Katika jedwali la migarazano hiyo, wanasoka wa Equity Bank bado wanazidi kufunza wapinzani wao jinsi ya kugaragaza gozi ya ng’ombe ambapo wangali kifua mbele kwa kutia kapuni alama 36, tano mbele ya Tandaza FC.
Nayo Shofco inafunga tatu bora baada ya kucheza mechi 16 na kukusanya pointi 30, moja mbele ya Alfones FC. Mbotela Kamaliza inafunga tisa bora kwa kuzoa alama pointi 18, moja mbele ya Uprising FC baada ya kusaka mechi 14 na 16 mtawalia. Kati ya wachezaji mahiri wa kikosi hicho, Jonadhan Nzuki anasema bado hawajayeyusha tumaini la kufuzu kushiriki kipute cha Ligi Kuu ndani ya miaka mitano ijayo.