Corona ilivyosambaratisha soka ya mitaani
NA JOHN KIMWERE
MKURUPUKO wa virusi vya corona unaendelea kuzuia shughuli za maisha kote duniani ikiwamo michezo.
Wadau wa mchezo huo nchini walikuwa na matarajio makubwa kwamba rais Uhuru Kenyatta angetoa tangazo la shughuli kurejea kawaida baada ya muda wa kafyu ya siku 21 kukamilika mwishoni mwa wiki.
Hatua hiyo imechanganya timu ambazo hushiriki vipute cha viwango vya chini hasa Ligi za Kaunti na Regional League awali zikifahamika kama Ligi za Mkoa.
Tangazo hilo bila kuweka katika kaburi la sahau hali tete inayoendelea kutikisa dunia nzima zimefanya timu husika kujikuta kwenye wakati mgumu bila kufahamu muda zitakaomaliza mechi za muhula huu.
”Buda janga la Corona limeleta ngori hasa wakati vijana walipokuwa fomu kujituma kiume kuwinda tiketi ya kupandishwa daraja,” amesema kocha wa Kibera Saints, William Mulatya na kuongeza kuwa kwa sasa hakieleweki.
Kibera Saints ni kati ya timu 21 zinaoshiriki kinyang’anyiro cha Nairobi West Regional League (NWRL). Andokeza kuwa athari za Corona zimevuruga kampeni za msimu huu maana hata virusi hivyo vikidhitibiwa ndani ya kipindi kilichoongezwa na serikali tayari mwaka umekwenda.
Anasema hali ya sasa itafanya timu za kijamii ambazo bado hazijapata wafadhili kuzipiga jeki kuendeleza za kukuza wachezaji chipukizi katika viwango vya mashinani.
Anasisitiza kuwa wameketi mkao wa subira kufuata mwelekeo utakaotolewa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) baada ya janga la Corona kudhibitiwa. Kampeni za michezo kote nchini zilipigwa breki pale kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kilipotangazwa mwezi Machi mwaka huu.
Corona inazua hofu kubwa kwa wachezaji wa vikosi vya soka katika mtaa wa Kibera maana ni kati ya maeneo yanayotikiswa na virusi hivyo.
”Tunatarajia kupata wakati mgumu hasa kwenye mechi zilizosalia zitakaporejea ingawa hatuelewi kitakaojiri kabla ya kukamilika kwa muda wa kafyu,” alisema John Mbenzwa kocha wa Kenya School of Government (KSG) maarufu Ogopa FC na kuongeza kuwa licha ya hali inayoendelea kwa sasa kikosi chake bado kinalenga kujitahidi kwa uvu na uvumba kupigania tiketi ya kusonga mbele.
Shughuli hizo zilisitishwa wakati vijana wa KSG walipokuwa wameanza kuonekana vingine kwenye kampeni za ngarambe hiyo. KSG Ogopa ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Kaunti ya Nairobi Magharibi kiulaini baada ya wapinzani wao MAA FC kuingia mitini na timu zote kufuzu kupanda ngazi.