Juhudi za kukuza soka ya wanawake zitazaa matunda – Akorot
Na JOHN KIMWERE
MENEJA wa kituo cha MYSA pia aliye mwanachama katika kamati ya kuteua waamuzi wa mechi za Ligi katika Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Maqulate Onyango Akorot amepongeza juhudi za shirikisho hilo za kukuza soka la wanawake nchini.
Anasema uongozi wa FKF ndani ya miaka minne iliyopita umeonyesha mwanga katika soka la wanawake kinyume na misimu iliyopita.
“Binafsi sina hofu kutaja kwamba FKF chini ya rais, Nick Mwendwa imeweka mikakati mizuri inayolenga kuinua kiwango cha mchezo huo nchini,” alisema na kuongeza kwamba viongozi waliotangulia wangeanza mapema Kenya ingekuwa imepiga hatua kubwa katika mchezo wa soka kimataifa.
Amesema kuwa mradi uliofadhiliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mwaka jana kutoa mafunzo kote nchini ulionyesha nia ya kupaisha kiwango cha mchezo huo mashinani.
Kupitia mradi huo FKF iliandaa semina za wakufunzi wengi tu wanaume na wanawake katika maeneo tofauti kote nchini.
Semina hizo ziliandaliwa katika maeneo tofauti ikiwamo Mombasa, Kisumu, Nairobi, Meru na mwisho Eldoret.
Anasema mkakati wa FIFA unalenga kusaidia wasichana ambao hushiriki soka la mashinani kujituma kwenye harakati za kupigania kufika kiwango cha kimataifa miaka ijayo.
Kadhalika alidokeza kuwa Kenya imeanza kuonyesha dalili za kupaisha soka la wanawake baada ya kufuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Afrika (AFCON).
Maqulate alifunguka hayo siku chache baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa Harambee Starlets, Richard Kanyi kutaja kuwa Kenya inakaa vizuri kufuzu kushiriki Olimpiki ama fainali za Kombe la Dunia.
Kenya ililemewa kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki zilizoratibiwa kuandaliwa mwaka huu baada ya kuzimwa na Zambia kwenye mechi za mkondo wa nne.
Kanyi alidokeza kuwa soka la wanawake limefaidi pakubwa ndani ya miaka mine iliyopita. ”Binfasi nashukuru uongozi wa FKF maana umechangia mabadiliko makubwa katika soka la wanawake.
Nimetambua kwamba tukiendelea kupata ufadhili na uungwaji mkono tunaweza kupiga hatua zaidi katika mchezo huo,” Kanyi akasema na kuongeza kwamba Mwendwa akipewa hatumu nyingi anaona dalili za Kenya kufanya kweli na kufuzu kushiriki Olimpiki.
Vile vile uongozi wa Mwendwa ulichangia pakubwa urejio wa Safaricom ambayo hufadhili mechi za Chapa Dimba na Safaricom ambazo ziliandaliwa mara nne kote nchini.
Chini ya uongozi wa sasa, Harambee Starlets kwa mara ya kwanza ilitwaa taji la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ilipochoma Tanzania mabao 2-0 katika fainali Uwanjani Chamazi jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Harambee Starlets chini ya kocha, David Ouma ililemea Tanzania iliyowahi kuwalima katika fainali ya kipute hicho mwaka 2016. Nao vipusa wa Crested Cranes ya Uganda waliibuka tatu bora walipozoa mabao 2-0 dhidi ya Burundi.