• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
ULIMBWENDE: Jinsi mwanamke anavyoweza kuzitunza nywele zake bila gharama kubwa

ULIMBWENDE: Jinsi mwanamke anavyoweza kuzitunza nywele zake bila gharama kubwa

Na MISHI GONGO

AGHALABU kila mwanamke mwenye kujiamini hupenda kuwa na nywele za kupendeza na zilizo na afya tele.

Lakini hali mbalimbali zikiwemo mazingira, hali ya afya, lishe, familia na kadhalika huwafanya baadhi ya wanawake kuwa na nywele hafifu zisizokuwa na mvuto. Utawaona wanawake wakinyonyoka au kukatika kwa nywele, wabisi, nywele kuwa kavu mno au kukosa kukuwa.

Kufuatia gharama kubwa za kuhudumiwa na wataalamu ili kurekebisha matatizo hayo, baadhi ya wanawake wamezumbua njia za kiasilia kupambana na matatizo hayo.

Njia ya kwanza ni kutumia maji ya Aloe vera yaani mshubiri.

Mtumiaji anapaswa kuchukua jani la mshubiri kisha kulipasua na kuvuna maji au ute wake.

Ute huo unapaswa kupakwa kwenye ngozi kichwani. Ute huo huwa na uwezo wa kuzizimisha ngozi na kwa mtu aliye na wabisi hupata afueni na kuondokewa na kadhia ya kujikuna.

Aidha Aloe vera inaaminika kumiliki virutubisho kama vitamini A, E na C ambavyo vinasaidia katika kukua kwa nywele na kuzitunza kuzuia zisikatike au kunyonyoka.

Bidhaa nyingine ambayo inasifika katika utunzaji wa nywele ni yai.

Kuna baadhi ya watu ambao huchanganya yai na asali na kupaka nyweleni kisha kuziacha kwa muda wa nusu saa ili kuzipatia nywele zao afya, kuondoa wabisi, kuzikuza, kuzizuia zisikatike na kuzifanya ziwe na rangi ya kupendeza.

Parachichi pia hutumika na walimbwende katika utunzaji wa nywele kutokana na uwepo wake wa mafuta asilia. Waliowahi kutumia tunda hili, husema hukuza nywele maradufu.

Kutumia parachichi mrembo anatakiwa kufanya rojo kisha kupaka katika nywele zake kutoka kwa mashina hadi ncha. Zinapokolea anayetumia hupaswa kuzifunika kwa mfuko au kofia kwa muda wa dakika 20 kisha kuosha kwa maji baridi.

Tui zito la nazi nalo pia linasifika hasa na watu wa Pwani katika kutunza nywele. Mwanamke anapaswa kukuna nazi kisha kuchuja tui zito na kulipasha moto hadi liwe vuguvugu. Baadaye likishapoa kiasi, analipaka katika nywele zake kutoka kwa mashina hadi ncha huku akikanda kichwa chake taratibu kuruhusu mzunguko wa damu. Anapomaliza shughuli hiyo, anaosha kwa maji fufutende.

Tui la nazi linasifika kwa kukuza nywele, kuzuia kukatika, kuondoa wabisi, kuzifanya ziwe nyororo na kuzifanya ziwe na rangi nyeusi iliyopasha au iliyokoleza.

You can share this post!

Jinsi ya kutumia viungo asili kuondoa harufu mbaya kwapani

Serikali ya udikteta

adminleo