Michezo

Real yaitaka Arsenal kuamua kuhusu hatima ya Auba

June 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

REAL Madrid wamewapa Arsenal hadi Juni 15, 2020 kufanya maamuzi kuhusu iwapo wanatarajia kumtia nahodha wao Pierre-Emerick Aubameyang mnadani au la.

Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real ni miongoni mwa vikosi vya haiba kubwa barani Ulaya ambavyo kwa sasa vinakeshea maarifa ya fowadi huyo matata mzawa wa Gabon.

Kufikia sasa, Aubameyang ambaye alitua ugani Emirates mnamo 2018 baada ya kuagana na kikosi cha Borussia Dortmund nchini Ujerumani, amesalia na miezi 13 pekee katika mkataba wake na Arsenal.

Kwa mujibu wa Pierre-Francois ambaye ni wakala wa Aubameyang, nyota huyo hayuko tayari kurefusha kandarasi yake ugani Emirates, jambo ambalo linawasaza Arsenal na maamuzi ya ama kumtia mnadani mwishoni mwa msimu huu au kumwacha atue anakotamani kwenda bila ada yoyote baada ya msimu wa 2020-21.

Kati ya mikakati ambayo Real imepania kutumia ili kujinasia huduma za Aubameyeng ni kuwapa Arsenal kiasi kidogo cha fedha pamoja na kiungo Dani Ceballos ambaye kwa sasa anahudumu uwanjani Emirates kwa mkopo kutoka kambini mwa miamba hao wa soka ya Uhispania.

Kubadilishana wachezaji kunatarajiwa kuwa biashara kubwa miongoni mwa vikosi vya bara Ulaya katika muhula ujao wa uhamisho hasa ikizingatiwa hasara ambayo imekadiriwa na klabu zote duniani kutokana na janga la corona msimu huu.

Iwapo Ceballos atapania kuondoka Arsenal kama ambavyo amefichua tayari, basi Real watalazimika kufungulia mifereji yao ya fedha na kuweka mezani kima cha Sh5.6 bilioni kwa minajili ya Aubameyang ambaye pia ni andazi moto kambini mwa Barcelona (Uhispania), Chelsea (Uingereza) na Inter Milan (Italia).

Akihojiwa na gazeti la The Sun, Zidane alidokeza pia uwezekano wa kumtuma Ceballos hadi Sevilla katika juhudi za kufanikisha mipango ya kumsajili kiungo Lucas Ocampos.