De Bryune na Sterling kugura Man City
LONDON, UINGEREZA
KOCHA wa Pep Guardiola wa Manchester City amesisitiza kuwa hana tatizo lolote kuhusu hatua ya viungo Raheem Sterling na Kevin De Bruyne kuibua mjadala unaowahusisha na uwezekano wa kubanduka ugani Etihad mwishoni mwa msimu huu.
Katika mahojiano yake na gazeti la AS nchini Uhispania mnamo Jumamosi, Sterling, 25, alikiri kuwa anayafurahia maisha yake uwanjani Etihad ila atakuwa radhi kukabiliana na changamoto mpya kwingineko iwapo marufuku inayowazuia Man-City kushiriki kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa miaka miwili ijayo itadumishwa.
Kwa upande wake, De Bruyne ambaye ni raia wa Ubelgiji aliliambia gazeti la HLN nchini Uingereza kwamba atahiari kuyoyomea Barcelona au Real iwapo Man-City watasalia nje ya kivumbi cha UEFA.
“Wanasoka wa Man-City wako huru kusema lolote wanalofikiria. Hatupo hapa kuwaelezea kuhusu nini cha kusema na kipi cha kubana,” akatanguliza.
“Real na Barcelona ni miongoni mwa klabu ambazo hutetemesha kila mtu iwapo zitaamua kuandamana mchezaji wa kikosi fulani kutokana na ushawishi wao wa kifedha,” akaongeza Guardiola kwa kukariri kwamba atakuwa tayari kurefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa Man-City baada ya 2021 licha ya maarifa yake kuwaniwa na Juventus.
Sterling aliingia katika kundi la wachezaji walio na ushawishi zaidi uwanjani Etihad mnamo Julai 2016 baada ya kuagana na Liverpool kwa kima cha Sh6.8 bilioni.
“Hakuna yeyote anayejua ya kesho. Mimi ni mchezaji na nitakuwa tayari kutafuta hifadhi mpya kwingineko iwapo fursa itajipa. Ingawa hivyo, kwa sasa nina mkataba na Man-City na hilo ni jambo ambalo nastahili kuliheshimu,” akasema Sterling kwa kusisitiza kwamba Real ni klabu ambayo ametamani sana kuichezea tangu utotoni mwake.
“Miaka miwili bila kusakata gozi la UEFA ni muda mrefu sana. Nasubiri kujua hatima ya Man-City katika kipute hicho kabla ya kutathmini ofa zitakazotokea,” akasema De Bruyne ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Chelsea na VfL Wolfsburg.
Mkataba wa sasa kati ya Sterling na Man-City unatazamiwa kukatika rasmi mwishoni mwa 2023. Guardiola, 49, aliingia kambini mwa Man-City mnamo 2016 baada ya kunyanyulia Bayern Munich ya Ujerumani mataji saba chini ya kipindi cha miaka mitatu.
Kufikia sasa, anajivunia kushindia Man-City mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza, matatu ya League Cup na Kombe la FA.
Mnamo Februari 2020, Man-City walitozwa faini ya Sh3.5 bilioni na kupigwa marufuku ya kushiriki kivumbi cha UEFA baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka sheria za Uefa zinazohusiana na masuala ya matumizi ya fedha na leseni.
Ingawa hivyo, walikata rufaa na wamekuwa wengi wa matumaini kwamba maamuzi hayo yatabatilishwa na mahakama ya kimataifa ya kushughulikia migogoro ya michezo.
Iwapo marufuku dhidi ya Man-City itadumishwa na mahakama ya mizozo ya michezo duniani, kikosi hicho huenda pia kikapunguziwa alama katika kipute cha EPL msimu huu, kwa sababu sheria za udhibiti wa masuala ya fedha katika kivumbi cha EPL kwa kiasi kikubwa, zinawiana na kanuni za Uefa, japo hazifanani moja kwa moja.
Pigo kubwa zaidi ambalo huenda likawapata Man-City ni ulazima wa kujisuka upya iwapo watakatiza uhusiano na Guardiola pamoja na masogora wengi wa haiba kubwa iwapo watazuiliwa kunogesha gozi la UEFA.
Mbali na De Bruyne na Sterling, nyota wengine ambao huenda wakaagana na Man-City ni Ederson Moraes, Sergio Aguero, Bernardo Silva na Riyad Mahrez.