Michezo

Hatujaathiriwa na corona – Ulinzi Stars

June 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MAKOCHA wa vikosi mbalimbali vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) wanapohofia uwezekano wa kushuka kwa viwango vya ubora wa wanasoka wao, Dunstan Nyaudo ambaye ni mkurugenzi wa benchi ya kiufundi wa Ulinzi Stars hababaiki kabisa.

Nyaudo amefichua kwamba mabingwa hao mara nne wa taji la KPL hawajaathiriwa sana na agizo la serikali la kusitisha shughuli zote za michezo na kupiga marufuku mikutano yote ya umma.

Kwa mujibu wa kinara huyo, mazoezi ya mara kwa mara yanayofanywa na wanajeshi katika kambi zao yamechangia kudumisha fomu za wanasoka wake wakati huu ambapo ulingo wa spoti umelemazwa na janga la corona.

Kocha huyo wa zamani wa Ulinzi Stars amesema kwamba japo masogora wao walirejea katika kambi zao mbalimbali za kijeshi baada ya shughuli za michezo kusimamishwa humu nchini, benchi ya kiufundi bado inatekeleza majukumu yake kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.

Amekiri kwamba wachezaji hupata mafunzo ya kila siku kutoka kwa kocha, hatua ambayo imepania kupiga jeki mazoezi ya kijeshi ambayo huendeshwa na katika kambi mbalimbali za humu nchini.

Kulingana na Nyaudo, kutokuwepo kwa mchezaji yeyote ambaye si mwanajeshi kambini mwa Ulinzi Stars pia kumechangia nafuu yao kwa kuwa wanasoka wao wote huwekwa katika ulazima wa kushiriki mazoezi na kambi zao za kijeshi na ni rahisi zaidi kufuatilia maendeleo yao.

“Kushiriki mazoezi ya pamoja bado ni changamoto. Hata hivyo, wachezaji wetu wana bahati kwa kuwa hujifanyia mazoezi kambini, ni rahisi kuwafuatilia na kuna wepesi mkubwa katika kuwapa miongozo ya kujifua kadri tunavyopania kupiga jeki taratibu za kawaida katika kambi za kijeshi,” akatanguliza.

“Hii husaidia kuwaweka fiti licha ya kanuni mpya za serikali kuhusu jinsi ya kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona. Tuna bahati kwamba hatukuwa na mwanasoka yeyote asiye mwanajeshi kikosini wakati kisa cha kwanza kabisa cha ugonjwa wa corona kiliporipotiwa humu nchini,” akasema Nyaudo.

Hofu ya pekee ya Nyaudo ni kuhusu fowadi Oscar Wamalwa anayetarajiwa kuanza mazoezi mnamo Agosti baada ya kupata jeraha la bega mnamo Februari 2020.

Wamalwa aliwafungia Harambee Stars mabao matatu mwaka jana na kuibuka mfungaji bora kipute cha Cecafa Senior Challenge nchini Uganda.