ONGAJI: Hatimaye tutalazimika kulegeza masharti ya corona
Na PAULINE ONGAJI
TAKRIBANI miezi mitatu baada ya janga la maradhi ya Covid-19 kuchipuka, virusi vya corona bado vinaendelea kuhaingaisha ulimwengu wote huku visa zaidi vikiendelea kunakiliwa.
Lakini licha ya haya, ukweli wa mambo ni kwamba mataifa mengi, Kenya ikiwa miongoni mwao, yatalazimika kulegeza misimamo mikali ya kupambana na virusi hivi, kwani wanasayansi wanasema kuwa maradhi haya hayaendi popote wakati wowote hivi karibuni.
Katika harakati hizi, kuna mambo tofauti ambayo sisi Wakenya tunapaswa kujifunza kutokana na masaibu ambayo tumepitia wakati huu wote.
Kwanza, Kenya ina uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali hasa za matumizi ya kiafya badala ya kuendelea kutumia kitita kikubwa cha pesa kuziagiza kutoka nje.
Tatizo ni kwamba sekta ya viwanda na uzalishaji bidhaa nchini imesakamwa na ukiritimba.
Pili, Kenya sawa na mataifa mengine ya Afrika, inastahili kuwekeza zaidi katika sekta ya sayansi na utafiti, badala ya kuelekeza macho kwa mataifa ya magharibu kwa majibu kila wakati ulimwengu unapokumbwa na janga la aina hii.
Ninasema hivi kulingana na jinsi ugonjwa huu ulivyotufanya sisi Waafrika kuonekana dhaifu kimawazo, na kutegemea taarifa kuhusiana na maradhi haya, kutoka kwa mataifa yaliyostawi.
Tatu, mataifa ya magharibi hayana kila suluhu kwa jambo au janga lolote linaloikumba ulimwengu, kwani tumeona baadhi ya nchi zilizostawi zikisumbuka na kushindwa kudhibiti makali ya virusi vya corona.
Kwa wanafunzi wanaosomea udaktari sio tu hapa Kenya, bali katika bara la Afrika, mojawapo ya masomo muhimu ya kusomea ni virolojia. Kwa nini nasema hivi? Katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita, Afrika imekuwa ikikumbwa na mikurupuko ya virusi mbalimbali, na wakati umewadia kwa wanasayansi wetu kuchangia pakubwa ili kupata suluhisho la tatizo hili.
Japo ni mapema kusema kwamba mawimbi ya corona yamepita, ukweli ni kwamba Afrika, ikilinganishwa na mabara mengine, imenakili visa vichache vya maambukizi na vifo kutokana na maradhi haya.
Hii inaonyesha kwamba Afrika kama bara ina uwezo wa kukabiliana na changamoto nyingi, na hivyo haya ni matumaini kwa bara hili ambalo kwa miaka limesemekana kuwa chimbuko la maradhi.
Zaidi ya yote, maradhi haya bila shaka yamekuwa funzo kwa Wakenya wenye mazoea ya kuchagua wanasiasa kwa misingi ya kikabila.
Kwanza, wametambua kwamba kabila sio kigezo muhimu cha kutathmini utendakazi wa kiongozi, na makosa haya ambayo tumerudia kwa miaka yameathiri miundomsingi katika sekta mbalimbali nchini, ya afya ikiwa miongoni mwazo.
Pili, ni raia yupi atakayekiri kwamba kuna mwanasiasa aliyebisha mlango wake na kutaka kumsaidia wakati huu mgumu eti kwa sababu yeye ni wa kabila lake?