• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Morans kuanza kujifua tayari kwa Afro-Basket licha ya marufuku

Morans kuanza kujifua tayari kwa Afro-Basket licha ya marufuku

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Cliff Owuor wa timu ya taifa ya mpira wa vikapu almaarufu Morans, anatathmini uwezekano wa kuanza kushiriki vipindi kadhaa vya mazoezi ya pamoja na baadhi ya wachezaji wa kikosi chake licha ya masharti yanayoharamisha mikusanyiko ya umma kuongezwa kwa siku 30 zaidi.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba idadi kubwa ya wanavikapu hao wataendelea kujifanyia mazoezi nyumbani kadri wanavyojiandaa kwa mechi za kufuzu kwa kipute cha Afro-Basket mnamo Novemba 2020.

“Licha ya kanuni zilizopo za kudhibiti maambukizi zaidi ya corona, wachezaji wana ulazima wa kusalia katika hali shwari na kudumisha ubora wa fomu. Haya ni mambo yanayowezekana iwapo kila mmoja atashiriki mazoezi ya viungo vya mwili,” akasema.

Owuor amesema atafichua ratiba itakayowaongoza wanavikapu wake kushiriki mazoezi ya pamoja katika vikundi vidogo vidogo kwa awamu.

“Yawezekana tuwe na makundi ya wachezaji wachache wakishiriki mazoezi huku wakizingatia kanuni zote zilizopo za afya ikiwemo kudumisha umbali wa mita moja kati yao,” akaongeza.

Kocha huyo ambaye anapanga kuwakutanisha wachezaji wake kwa mechi za kirafiki dhidi ya Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya corona kudhibitiwa vilivyo, ana wingi wa matumaini kuwa kikosi chake kitafaulu vyema kwenye mechi za kufuzu kwa fainali za Afro-Basket.

“Tuna nafasi maridhawa ya kufuzu kwa raundi ya mwisho. Hata hivyo, inatupasa kujituma vilivyo mazoezini na kujifua kabisa hasa ikizingatiwa ubabe wa wapinzani tutakaovaana nao Novemba,” akasema.

Kenya imepangiwa kumenyana na mabingwa wa bara la Afrika Angola, Msumbiji na Senegal katika kundi la timu nne zitakazocheza michuano ya mikondo miwili; yaani nyumbani na ugenini.

Viwanja vitakavyotumiwa kuandalia mechi hizo bado havijathibitishwa.

Nahodha wa Kenya Griffin Ligare, amesema kikosi huandaa vikao vya mara kwa mara mitandaoni kwa minajili ya kutiana hamasa na kufuatilia miongozo ya kushiriki mazoezi inayotolewa na kocha.

You can share this post!

Wazee sita huuawa kila wiki Pwani – Serikali

Duale motoni tena

adminleo