Michezo

Bingwa wa Cardiff Marathon awapa wanariadha nyumba zake za kukodisha bwerere

June 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa zamani wa Cardiff Half Marathon, John Kipsang Lotiang, amewapa wanariadha ambao wameathiriwa zaidi na janga la corona nyumba saba za kukodisha bila malipo.

Mwanariadha huyo mzawa wa Pokot Magharibi ametoa bure jumla ya nyumba saba za aushi na za kisasa alizozijenga katika eneo la Mororia, kilomita tatu kutoka mjini Iten. Nyumba hizo zilizokamilishwa kujengwa wiki mbili zilizopita, zitawapa hifadhi watimkaji ambao kwa sasa wanatatizika pakubwa kupata makao au kulipa kodi wakati huu mgumu wa hali ya kiuchumi.

“Najua jinsi baadhi ya wanariadha wenzangu, hasa chipukizi, wanavyoteseka kwa sasa baada ya mapambano ambayo ni kitega-uchumi cha pekee kwao kusitishwa na janga la corona. Wengi wao hawana mpango mbadala wa kujikimu kimaisha baada ya kambi zote kuvunjwa na ninatumai kwamba msaada huu nilioutoa utawafaa sana kwa kipindi hiki kabla ya corona kudhibitiwa vilivyo,” akasema Lotiang.

Hata hivyo, hajafichua mfumo atakaotumia kuteua wanariadha watakaonufaika na msaada wake huo hasa ikizingatiwa kwamba zaidi ya kambi 140 za mazoezi ya wanariadha katika kaunti za Pokot, Uasin Gishu na Elgeyo-Marakwet zimefungwa.

Lotiang aliibuka mshindi wa mapambano mengi mwaka jana na amewataka wanariadha wengine walio na moyo na uwezo kuchangia wenzao kwa njia yoyote wakati huu.

“Kugawa kidogo tulichonacho ni ishara ya uanaspoti mwema. Napania sasa kutoa sehemu fulani ya mapato ya kifedha niliyojizolea kutokana na ushindi wangu kwenye mapambano mbalimbali kwa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) ili msaada huo uwafikie wanariadha wanaostahili,” akaongeza Lotiang aliyeambulia nafasi ya nne kwenye Half Marathon ya Jumuiya ya Madola iliyoandaliwa jijini Gold Coast, Australia mnamo 2018.

Lotiang ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya Cardiff City Half Marathon, alitarajiwa kujitosa kwenye mbio za kilomita 42 kwa mara ya kwanza mwaka huu kwa kushiriki Wuhan Marathon, China.

Baadaye, alitazamiwa kunogesha Istanbul Half Marathon na Ottawa Marathon mtawalia. Mbio hizo zote zilifutiliwa mbali mwaka huu.

Lotiang alichaguliwa kuwakilisha Kenya kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2018 baada ya kuvunja rekodi ya Cardiff Half Marathon kwa kusajili muda wa dakika 60:40 mnamo 2017.