AKILIMALI: Sharubati yake ya miwa ni tiba na yamkidhia mahitaji
Na PETER CHANGTOEK
DANIEL Gitari amekuwa akishughulika na ukuzaji wa miwa na usindikaji wa zao hilo ili kutengeneza sharubati ya kipekee ambayo anafichua kuwa ina uwezo wa kutibu magonjwa kadha wa kadha.
Yeye ni maarufu mno kwa wakazi wanaosakini katika janibu za mji wa Kutus, katika Kaunti ya Kirinyaga.
Mkulima huyo alijitosa katika shughuli hiyo miaka minane iliyopita, na hana nia yoyote ya kuacha shughuli hiyo hivi karibuni wala hatazami nyuma.
“Nilianza kutekeleza mradi huu baada ya kugundua kwamba watu huwa na matatizo ya muda mrefu kupata kinga, hasa yale yanayotokana na dawa za kawaida,” aeleza mkulima huyo.
Gitari, ambaye amewahi kuhudhuria mafunzo na semina mbalimbali nchini na katika nchi nyinginezo mathalani; China na India, alianza kutengeneza shurubati hiyo yenye tiba, anayosema hutibu maradhi kama vile shinikizo la damu, magonjwa ya figo, jongo (arthritis) miongoni mwa magonjwa mengine, ili ku wapa wenye matatizo hayo suluhisho.
Kinywaji hicho ni maarufu katika eneo hilo kama kiboti au ‘kifagio’ kwa sababu kina uwezo wa ‘kufagia’ magonjwa kutoka mwilini.
Yeye huanza shughuli zake wakati wa majogoo; saa kumi alfajiri ili kutayarisha viungo.
Kwa wastani, yeye huwahudumia wateja kati ya 200 na 400 kwa siku, na ifikapo wakati wa adhuhuri, sharubati hiyo huwa imeisha.
Gitari, mwenye umri wa miaka 60, huikuza miwa katika shamba ekari tano analolikodi kutoka kwa watu wengine. Mbali na kufanya hivyo, yeye amewapa kandarasi
wakulima kadhaa kuikuza miwa ili wamuuzie kusudi asiwe na uhaba wa malighafi hiyo muhimu.
Aidha, mkulima huyo amewapa kandarasi wakulima wengineo kuikuza mimea ya viungo kama vile mishubiri (aloe vera), vitunguu saumu, mimea ya ‘pepino’, mitango (cucumbers) n.k.
Isitoshe, yeye huvinunua viungo kama vile mdalasini kutoka Uganda na Tanzania, japo ni changamoto kuvipata wakati huu ambapo pana gonjwa la korona.
Kila wiki, Gitari huinunua miwa 3,000 kwa Sh15-Sh20 kila mmoja. Miwa hiyo, ambayo hujaa kwa lori moja, hutumika kwa muda wa wiki moja kutengeneza sharubati.
Ili kumudu kazi shambani na katika eneo la kutengenezea sharubati, mkulima huyo ana wafanyikazi 15 – kumi kati yao ni wa kudumu ilhali watano ni vibarua.
Kila siku yeye hutengeneza sharubati kwa mujibu ya oda za wateja.
“Watu wana hali tofauti za afya zinazolazimu sharubati zenye tiba tofauti tofauti itengenezwe. Kwa mfano, kwa wale wenye vidonda tumboni au gesi; kiungo kikuu kinachotakikana ni shubiri, kwa wale wenye mizongo ya akili inayoambatana na kupoteza fahamu; kiungo kikuu ni matango,” asema Gitari.
Anaongeza: “Kwa wale wenye kolestro; kiungo ni limau na tangawizi, ilhali kwa wale wenye magonjwa ya figo; tangawizi na shubiri ni muhimu.”
Kwa wale wenye shida ya upungufu wa nguvu za kiume na shida za kuzalisha, mkulima huyo hutumia mihogo na majani megineyo.
Alianzisha shughuli hiyo kwa kuutumia mtaji wa sh500,000 – pesa taslimu ambazo alizitumia kununua mashine ya kutengeneza juisi, jenereta na kukodi mahali pa kufanyia biashara.
Gitari, ambaye anasema kuwa ana leseni zinazomruhusu kuhudumu, huuza sharubati yake katika kaunti za Nyeri, Nairobi, Meru, Embu, Murang’a, Kirinyaga na viunga vyake.
Sharubati hiyo inaweza kuhifadhiwa kwa maji baridi ili ikae kwa muda wa siku tatu au ihifadhiwe kwenye jokofu ili idumu kwa muda wa wiki moja.
Mkulima huyo hufanya utafiti ili kuboresha bidhaa zake. Yeye hupata kati ya Sh5,000 na Sh10,000 kwa siku.