Habari

Bajeti yanyonga wanyonge

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

BAADA ya virusi vya corona kuvuruga maisha ya mamilioni ya wanyonge nchini, Serikali imezima matumaini yao kupumua baada ya bajeti iliyosomwa Alhamisi kupendekeza kuongezwa kwa bei za vyakula na bidhaa zingine muhimu zaidi.

Kwa mujibu wa Mswada wa Fedha 2020 unaoeleza jinsi Serikali itakavyofadhili bajeti ya 2.7 trilioni, Waziri wa Fedha Ukur Yatani, alipuuza kilio cha walala hoi kutokana na ugumu wa maisha magumu wanayopitia, na badala yake akapendekeza mzigo mkubwa zaidi kwao.

Wazee na vijana pia hawana afueni kwani seikali imetangaza nia ya kuwapunguzia kidogo wanachopata kwenye pensheni na biashara za kidijitali mtawalia.

Serikali pia imepiga abautani katika sera zake za kulinda mazingira na utimizaji wa ajenda ya umiliki nyumba kwa gharama nafuu pamoja na ustawishaji wa kilimo.

VAT KWA CHAKULA

Ushuru wa VAT unaopendekezwa kutozwa bidhaa za kimsingi kama vile mahindi, unga wa ngano, maziwa, mayai na vyakula vinginevyo utapandisha bei ya bidhaa hizo wakati huu mgumu.

Kwa sasa bidhaa hizi hazitozwi ushuru huo, lakini wabunge wakipitisha mswada huo, unga wa mahindi unaotumika zaidi nchini utapanda kutoka Sh120 hadi Sh136 kwa pakiti ya kilo mbili.

“Japo Mswada huo wa Fedha haujatoa ufafanuzi, kurejeshwa kwa ushuru wa VAT kwa bidhaa za vyakula kutapandisha bei ya bidhaa hizi wakati huu ambapo mapato ya raia wengi yamepungua kutokana na janga la Covid-19,” anasema mtaalamu wa masuala ya uchumi Tony Watima.

Anaongeza kuwa kwa serikali kupanga kuanza kutoza ushuru wa asilimia 14 kwa bidhaa za kilimo kama vile trakta, gharama ya kilimo itapanda.

“Hii itaenda kinyume na azma ya serikali ya kufanikisha ajenda ya utoshelezaji wa chakula kufikia mwaka wa 2022,” Bw Watima anaeleza.

BEI YA GESI YA KUPIKIA JUU

Mswada huo pia unapendekeza kutoza ushuru wa VAT wa asilimia 14 kwa gesi ya kupikia, hatua ambayo itachangia kupanda kwa bei bidhaa hiyo.

Hii ina maana bei mtungi wa kilo 13 wa gesi itapanda kutoka Sh2,200 hadi Sh2,552 jijini Nairobi.

Wale ambao wangegeukia jiko za makaa zinazotumia moto kidogo (eco jiko), pia hawana pa kukimbilia kwani viwanda vya kutengeneza jiko hizo sasa zitaanza kutozwa ushuru wa VAT wa asilimia 14.

Hatua hizi kuhusu gesi na jiko zinamaanisha gharama ya kupika kwa wananchi wa kawaida itaongezeka kwa kiwango kikubwa.

Vibarua walio na bidii kwa kufanya kazi ya ‘overtime’ nao wataanza kutozwa pesa za ziada wanazopata, hali itakayofanya maisha yao kuwa magumu zaidi.

Kwa sasa, watu wanaopata mshahara wa chini ya Sh12,298 huwa hawatozwi ushuru kwa pesa za ‘overtime’ ama marupurupu mengine wanayolipwa.

“Ikitiliwa maanani ugumu wa maisha kutokana na Covid-19, Serikali haingetoza ushuru pesa za ziada kwa watu wa mishahara ya chini, ambao wengi hupokea marupurupu hayo kutokana na bidii yao,” ikasema ripoti ya uchanganuzi wa bajeti ya kampuni ya uhasibu ya KPMG.

Pigo jingine ni kwa wazee walio na miaka 65 na zaidi kwani sasa pesa zao za uzeeni wanazopokea kila mwezi zitaanza kutozwa ushuru.

Hii ni licha ya kuwa wazee hao ni miongoni mwa wanaotambuliwa na Serikali katika mpango wa “Inua Jamii”, na huwa wanapokea Sh2,000 kila mwezi.

USHURU WA PENSHENI

Hatua hii ya kutoza ushuru penseni yao itakuwa ni sawa na kuwapa kwa mkono mmoja na kuwapokonya kwa mwingine, kumaanisha hawatakuwa wamesaidiwa.

Masaibu ya wazee hayajaisha kwani mswada huo pia unapendekeza ushuru wa asilimia 25 uwe ukitozwa pesa za NSSF mfanyikazi anapostaafu.

Hatua hii itapunguza mapato ya wanaostaafu, na pia ni kinyume cha sheria ambayo inazuia utozaji ushuru wa mapato ya hazina za uzeeni zilizosajiliwa.

Ajenda ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu nyumba nafuu, nayo imehujumiwa. Hii ni baada ya Serikali kupendekeza kuondolewa kwa nafuu ya ushuru ya Sh96,000 ambayo imekuwa ikipewa wanaowekeza kwenye hazina za nyumba.

Akiba zao pia sasa zitaanza kutozwa ushuru wa mapato baada ya kupendekezwa kampuni wanakowekeza zianze kulipa kodi.

Hii itapunguza mapato ya wawekezaji na kuwafanya kushindwa kutimiza ndoto zao za kumiliki nyumba.

Kufikia sasa zaidi ya watu 20,000 wameweka akiba ya zaidi ya Sh230 milioni chini ya mpango wa Serikali wa “Boma Yangu”.

Ikiwa wabunge watapitisha mswada huu, zaidi ya watu 300,000 ambao wamejisajili tayari kujiunga na mpango huu watavunjika moyo.

Wanaokodisha nyumba pia sharti wakaze mishipi kwani kodi itapanda kuanzia Julai mswada wa Bw Yatani ukipita.

KODI YA NYUMBA KUPANDA

Hii ni kutokana na pendekezo la kuongeza ushuru unaotozwa mapato kutokana na nyumba za kukodisha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15.

Hii ina maana kuwa wamiliki wa nyumba za makazi, na za kibiashara, watapandisha kodi kwa wateja wao.

Watu wanaoendesha biashara mitandaoni, wengi wao wakiwa vijana, pia hawana bahati kwani mapato yao yatatozwa ushuru wa asilimia 1.5.

Wenye biashara ambazo hazipati faida pia watakuwa wakilipa ushuru wa asilimia moja ya mauzo ya kila mwaka.