Wanariadha 6 wa Kenya kupokea Sh400,000 kila mwezi
Na CHRIS ADUNGO
WANARIADHA sita wa Kenya watanufaika kifedha kutoka kwa Kamati ya Olimpiki ya bara la Afrika (ANOCA). Ufadhili huo utawasaidia kujiandaa kwa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2021 jijini Tokyo, Japan.
Watakaonufaika ni bingwa wa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 800 Wycliffe Nyamal, mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za chipukizi za mita 10,000 kwenye Jumuiya ya Madola Rodgers Kwemoi, Emily Cherotich Tuwei wa mbio za mita 800 na mshindi wa medali ya shaba katika mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia, Ferguson Rotich.
Wengine ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Conseslus Kipruto na bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot.
Wanariadha hao watapokea Sh400,000 kila mmoja kwa kipindi cha miezi minne ijayo.
“Mfumo uliotumiwa kuwateua sita hawa ulikuwa wazi. Mwanariadha alitakiwa kuwa mshindi wa dunia katika fani yake msimu uliopita au kuorodheshwa wa kwanza katika kitengo chake barani Afrika,” akatanguliza Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Jackson Tuwei.
“Baada ya miezi minne, tutarejelea tena mzungumko wa kutoa Sh400,000 kwa kipindi kingine cha miezi minne hadi wakati wa Olimpiki mwaka ujao. Ilivyo, ufadhili huo utakatika Juni 23, 2021 takriban siku 30 kabla ya Olimpiki kuanza,” akaongeza kinara huyo.