Michezo

Kiungo wa Ingwe Marvin Nabwire apona majeraha

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha AFC Leopards kimepigwa jeki na kupona kwa kiungo wao matata Marvin Nabwire ambaye huenda akawakweza pazuri mwishoni mwa msimu huu iwapo kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) zitarejelewa baada ya masharti ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19 kulegezwa.

Nabwire amekuwa mkekani kuuguza msururu wa majeraha tangu Disemba 2018 alipoumia goti lililolazimu kufanyiwa upasuaji mnamo Aprili 2019.

Licha ya kurejelea mazoezi mepesi mnamo Novemba 2019 na kuanza kuwajibishwa katika baadhi ya mechi za Disemba 2019, Nabwire alikosa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Leopards baada ya kupata jeraha jingine la kifundo cha mguu mnamo Februari 2020.

Mwanafunzi huyo wa zamani wa Kakamega High alikuwa akipania kufuma wavuni angalau mabao 10 katika mechi za mkondo wa pili wa KPL mnamo 2019-20.

Hata hivyo, alipata jeraha la misuli ya miguu alipokuwa akicheza dhidi ya Kisumu All Stars na kuwekwa mkekani kwa kipindi kirefu.

Likizo ya lazima ambayo imechangiwa na janga la corona imekuwa nafuu kubwa kwa Nabwire ambaye kwa sasa atakuwa katika hali shwari ya kuwajibishwa kivumbi cha KPL kitakaporejea.

Shughuli zote za michezo na mikusanyiko ya umma imepigwa marufuku kwa sasa katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi ya corona.

“Nabwire amepona jeraha na tunatazamia akirejea kuwania upya nafasi yake kwenye safu ya kati ya Leopards,” akasema mwenyekiti wa Leopards, Dan Shikanda.