• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
RB Leipzig wazamisha Hoffenheim, wazidishia Dortmund presha

RB Leipzig wazamisha Hoffenheim, wazidishia Dortmund presha

Na CHRIS ADUNGO

DANI Olmo alifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza na kusaidia RB Leipzig kuzamisha Hoffenheim na hatimaye kupunguza pengo la pointi kati yao na Borussia Dortmund wanaoshikilia nafasi ya pili hadi alama moja pekee.

Leipzig kwa sasa wanakamata nafasi ya tatu kwa alama 62, nane nyuma ya viongozi Bayern Munich ambao wanafukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa msimu wa nane mfululizo.

Olmo aliwaacha hoi mabeki wawili wa Hoffenheim na kupachikwa wavuni bao la kwanza kunako dakika ya tisa, sekunde 120 kabla ya kufunga goli la pili kwa kombora alilolivurumisha kutoka nje ya kijisanduku.

Kikosi cha kwanza cha Leipzig kilijivunia pia huduma za fowadi Timo Werner ambaye anatarajiwa kuyoyomea ugani Stamford Bridge, Uingereza na kuanza kuvalia jezi za Chelsea mwishoni mwa msimu huu baada ya kusajiliwa kwa kima cha Sh7.4 bilioni.

Hoffenheim walipokezwa mkwaju wa penalti matokeo yakiwa 0-0 ila maamuzi hayo ya refa yakabatilishwa na VAR.

Werner ambaye tayari amefunga jumla ya mabao 25 katika Bundesliga msimu huu, alipoteza nafasi nyingi ambazo zingemwongezea idadi ya magoli kapuni mwake. Kwa wakati mmoja, alijipata akipaisha mpira juu ya mlingoti licha ya kusalia peke yake na kipa wa Hoffenheim.

Winga wa zamani wa Everton, Ademola Lookman pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Leipzig baada ya kutokea benchi katika kipindi cha pili.

Bayern Munich watatia kibindoni ufalme wa Bundesliga msimu huu leo iwapo watawachabanga Borussia Monchengladbach nao Dortmund wajikwae dhidi ya limbukeni Fortuna Dusseldorf.

You can share this post!

KIPWANI: Lil Mizze ataka wasanii Pwani washirikiane kufanya...

Barcelona yathibitisha Messi, Suarez na Umtiti wamepona

adminleo