• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
JAMVI: Baraka za Talai zadhihirisha jinsi ambavyo Wakalenjin ‘wamemshiba’ Uhuru

JAMVI: Baraka za Talai zadhihirisha jinsi ambavyo Wakalenjin ‘wamemshiba’ Uhuru

Na WANDERI KAMAU

NI dhahiri sasa huenda jamii ya Wakalenjin imemtema Rais Uhuru Kenyatta kama kiongozi wake, baada ya wazee wa ukoo wa Talai kumwidhinisha Naibu Rais William Ruto kama kiongozi mpya.

Kulingana na mila za Wakalenjin, Rais Kenyatta ndiye amekuwa kiongozi wa jamii hiyo tangu 2017, alipoidhinishwa na wazee hao ambao wanatoka katika jamii-ndogo ya Nandi.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto walikimbilia “usaidizi” wa wazee hao baada ya ushindi wao mnamo Agosi 8 kufutiliwa na Jaji Mkuu David Maraga.

Wachanganuzi wa tamaduni za Wanandi wanasema kuwa matambiko ya wazee hao huwa yenye nguvu sana na ndiyo maana wawili hao walishauriwa kutafuta usaidizi wa ghafla kutoka kwao, ili kuondoa mikosi yoyote ambayo ingewaandama.

Ni kwenye hafla ya haraka iliyofanyika katika Kaunti ya Nandi ambapo Rais Kenyatta aliidhinishwa kama kiongozi rasmi na msemaji wa jamii hiyo, huku Dkt Ruto akitawazwa kuwa naibu wake.

Wachanganuzi wa masuala ya kitamaduni wanasema kuwa ingawa kuna sababu zingine zilizochangia Rais Kenyatta kutangazwa mshindi kwenye duru ya pili ya uchaguzi huo wa mnamo Oktoba 26 na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), tambiko walilofanyiwa ni mojawapo ya sababu hizo.

Na kutokana na hatua ya Dkt Ruto kuidhinishwa rasmi na wazee hao kama kiongozi mpya wa Wakalenjin Ijumaa iliyopita, wadadisi wanasema kuwa huenda hafla hiyo ikaashiria rasmi kwamba jamii imemtema kisiasa Rais Kenyatta.

Kulingana na Dkt Godfrey Sang, ambaye ni mchanganuzi wa siasa na historia ya Wakalenjin, ukoo wa Talai huwa wenye ushawishi mwingi sana katika jamii hiyo, kwani wao ni uzawa wa Koitalel arap Samoei, aliyewaongoza Wanandi na Wakalenjin kwa jumla kuwakabili Waingereza walipoivamia ardhi yao.

“Ingawa Koitalel anatoka katika jamii ya Wanandi, anaheshimika sana na koo zote za Wakalenjin kutokana na mchango mkubwa ambao alitekeleza katika kuwazuia Waingereza kuvamia ardhi yao walipokuwa wakijenga reli kuu ya kutoka Mombasa hadi Kisumu mwanzoni mwa karne ya 20,” asema Dkt Sang.

Wachanganuzi pia wanasema tambiko hilo huenda linamaanisha kuwa Dkt Ruto tayari ameanza safari yake kisiasa kwa njia huru, kutokana na masaibu ambayo amekuwa akipitia katika serikali ya Jubilee tangu handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga mnamo Machi 2018.

“Baraka alizopokea Dkt Ruto kutoka kwa wazee hao zinamaanisha kwamba amepewa idhini ya kuanza safari yake huru. Hilo pia linalenga kumlinda dhidi ya mikosi yoyote ambayo huenda akakumbana nayo kwenye safari hiyo,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye pia ni mdadisi wa siasa za Bonde la Ufa.

Anasema kuwa kindani, tambiko hilo linafanana na baraka alizokuwa akipokea kiongozi wa jamii, alipokuwa akielekea kwenye vita, ambapo ziliendeshwa na wazee nyakati za asubuhi.

Wachanganuzi wa tamaduni za Kikalenjin wanasema kuwa baada ya kutawazwa kama kiongozi wa jamii hiyo mnamo 2017, Rais Kenyatta alivikwa taji la “Jemedari” aliyetwikwa jukumu la kuiongoza jamii kwenye vita, lakini ameasi jukumu hilo.

Uasi huo unafasiriwa kuwa mwenendo wa Rais Kenyatta kumtenga Dkt Ruto kwenye masuala muhimu yanayohusu uongozi wa nchi na kuwaondoa washirika wake kisiasa kwenye nyadhifa muhimu katika uongozi wa Seneti na Bunge la Kitaifa.

Rais vilevile anafananishwa na ‘jenerali’ aliyeiasi jamii baada ya kutumwa kwenye vita, kwa kuungana na ‘adui’ wao. Wadadisi wanasema kuwa kwa fasiri za kitamaduni, hilo ni kosa lenye uzito sana.

“Ingawa hatusemi kuwa Bw Odinga ni adui wa Wakalenjin, lililo dhahiri ni kuwa kwa muktadha wa kitamaduni, mkataba wa kisiasa wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto ulikuwa na upekee wake mkubwa. Hii ni kwa kuwa ulikitwa kwenye misingi ya kidini na kitamaduni, ingawa lengo lake kuu lilikuwa la kisiasa,” asema Bw Mutai.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto walibuni muungano wa Jubilee mnamo 2012 kwa kuviunganisha vyama vya TNA na URP katika uwanja wa Afraha mjini Nakuru, kutokana na mashtaka ya uhalifu wa kivita yaliyowakabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kufuatia ghasia za uchaguzi tata wa 2007/2008.

Lakini licha ya hayo, baadhi ya viongozi wanapinga vikali dhana ya tambiko hilo, wakitaja hafla ya ‘kutawazwa’ kwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto kama jambo la kawaida ambalo hufanyiwa wanasiasa.

Kulingana na mbunge wa Tiaty, William Kamket, Wakalenjin huwajakumbatia viongozi wengine kisiasa kama walivyomuunga mkono Bw Odinga mnamo 2007 na kumpa jina ‘Arap Mibei’. Vilevile, anapuuzilia mbali “uzito” wa wazee wa Talai, akisema kuwa hata jamii ya Watugen, anakotoka Seneta Gideon Moi (Baringo) vilevile huendesha hafla kama hizo.

Mbunge huyo ni mshirika wa karibu wa Bw Moi, ambapo anasisitiza kuwa ndiye kiongozi halisi wa Wakalenjin, hasa baada ya kukabidhiwa fimbo maalum (rigat) kwenye mazishi ya babake mnamo Februari.

You can share this post!

JAMVI: Vita vya ubabe kati ya Uhuru na Ruto vyahamia...

SIASA: ‘Minji minji’ wahisi joto

adminleo