Makala

Mambo unayoweza kuachana nayo ili uwe mwenye furaha maishani

June 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

HUWEZI kununua furaha dukani bali ni hali ambayo mtu huijenga na kuwa mwenye faraja.

Furaha ni kitu kinachotokana na mtu mwenyewe kuamua kuwa mwenye amani na hisia nzuri zitakazochangia awe na bila wasiwasi licha ya shida au matatizo aliyo nayo.

Furaha huleta matumaini na kumfanya mtu ajihisi huru na mwenye uwezo wa kufanya mambo makubwa.

Kwa bahati mbaya, si watu wengi wenye furaha labda hali hii ikitokana na sababu mbalimbali za kimaisha.

Unaweza kujaribu kuachana na mambo kadhaa ili uongeze furaha yako.

Kutaka kukubalika na watu

Usipende kutaka kila kitu unachofanya kikubalike au uungwe mkono na watu wengine; yaani usifanye furaha yako kuwepo tu pale unaposifiwa na mtu au watu fulani.

Katika maisha kuna watu tofauti hivyo si kila mtu ataona uzuri wa kila kitu unachofanya. Ni vyema ukaelewa kuna baadhi ya mambo unayofanya yatapendwa na mengine kuchukiwa. Lakini pia usisahau kujua kwamba katika ubaya wowote ulio nao – udhaifu wako – yupo mtu anakupenda bila kujali udhaifu wako huo.

Kuwa na hasira au kisirani wakati wote

Ni kawaida kukasirika pale unapochukia kitu, jambo au hali fulani. Ingawa hivyo, ni vizuri pia kufahamu kwamba hasira yako inaweza ikafanya uwe na ari ya kufanya jambo jema lenye faida kwako.

Mfano, kama hasira yako ni ya kutaka nawe uwe bora au kuwa vizuri kwa namna fulani, hilo ni jambo jema lakini ikiwa hasira zako ni za kubomoa na kukuletea hasara ni vyema kudhibiti mapema kabla ya kuzua balaa. Kikubwa ni kuweza kutumia busara zako na kuweza kudhibiti hasira zako zinazokusuma kufanya mabaya zisikutawale.

Kutojikubali uzuri wa mwili wako

Kuna mtu mmoja tu wa kukufanya ujithamini, kujiona na kujikubali kuwa wewe yu’ kiumbe bora.

Mtu huyo mmoja ni wewe. Uzuri wako unaujua wewe mwenyewe hivyo jivunie kuwa wewe, usifanye furaha yako kupatikana baada ya kusifiwa na watu wengine. Jivunie kuwa wewe. Jipende na penda kila kitu kuhusu akili yako na mwili wako.

Kutaka kuwa na rafiki au mpenzi mkamilifu

Hakuna binadamu aliyekamilika, hakuna mtu asiye na udhaifu. Jifunze kukubali na kuwachukulia watu jinsi walivyo. Huwezi kumbadilisha mtu awe utakavyo wewe ila watu hubadilika wanapoamua kubadika wenyewe. Kama unataka mtu abadilike mtendee mambo mazuri na onyesha upendo wako kwake kwa kumueleza mambo mazuri ambayo ungependa awe. Mueleze taratibu kwa upendo nini ajirekebishe au nini afanye ili kuwa mtu bora kwa namna unavyoona inafaa.

Kuona maisha yana usawa

Ni vyema kuelewa kuwa maisha hayana usawa.

Nasema hivyo kwa maana licha ya jitihada tunazofanya ili tufanikiwe katika malengo na matarajio yetu sio kila kitu kitakwenda vizuri.

Kuna kushindwa, kupata mapungufu ya hapa na pale au kutokuwa na bahati kwa namna ulivyotegemea.

Kufikiria sana mambo yaliyopita

Huwezi kubadilisha mambo yaliyopita. Ikiwa unajutia au kujilaumu kwa lolote lililotokea zamani, ni vyema ukajitahidi kuondoa mawazo hayo. Ishi kwa wakati wa sasa, usiwe ‘mtu wa kale’ na pia usihofu yajayo. Kama ukiamua kujenga maisha yako sasa kwa furaha na kujiwekea malengo madhubuti kwa nia ya kuwa na maisha bora hapo baadaye, ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa mazuri zaidi na furaha yako itaongezeka zaidi.

Kuwa na wivu uliopitiliza

Wivu ni hisia nzuri ikiwa mtu ataweza kujitawala na kujidhibiti asizidishe hisia zake zikapitiliza kawaida. Sote tumeona wivu katika mapenzi unavyoweza kuwa ni kitu kizuri chenye kuashiria upendo lakini pia wivu unaweza kuwa ni kitu kibaya kinachoweza kumchochea mtu kufanya mambo mabaya.

Wivu ni adui wa furaha. Acha kumwonea wivu mwenzako na badala yake jifunze kutoka kwake ni mbinu gani ametumia kuwa hivyo unavyomuona. Kumbuka hata wewe una yako mazuri ambayo watu hukuonea wivu.

Mambo haya ni baadhi tu ya mambo unavoweza kufanya kujiongezea furaha maishani.