• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 3:23 PM
Re Union yajiandaa kwa msimu ujao

Re Union yajiandaa kwa msimu ujao

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Re Union FC inapania kujituma kiume kwenye mechi za Nairobi West Regional League (NWRL) muhula ujao. Re Union inaorodheshwa kati ya klabu kongwe hapa nchini pia zilizona historia pevu katika soka la hapa Kenya.

Re Union inaonekana imekaa pazuri katika jedwali la kipute cha mechi za Kundi Ligi ya Kaunti ya Nairobi. Katibu wake, Caleb Ochieng Mumbo anasema ”Bila shaka kulingana hali ilivyo kwa sasa tunatarajia kupokezwa tiketi ya kupanda ngazi kushiriki mechi za NWRL msimu ujao.”

Aliongeza kuwa ingawa hawajacheza mechi zote kumi za mkumbo wa kwanza tayari wamo nafasi nzuri kusonga mbele. Katibu huyo amesema hayo kufuatia hatua iliyochukuliwa na FKF kumaliza kipute cha Ligi Kuu ya KPL.

”Katika mpango mzima timu zote zimeanza kupiga hesabu kulingana na msimamo wa ligi zinazoshiriki,” alisema mwenyekiti wa klabu hiyo, Charles Omollo Tude na kuongeza kuwa ingawa nafasi ya kupandishwa ngazi inachangiwa na mlipuko wa virusi hatari vya corona bado wangefanikiwa kushinda tiketi ya kusonga mbele.

Re Union ambayo hunolewa na kocha, Joseph Milimo inashikilia nafasi ya pili kwa kukusanya pointi 21 baada ya kucheza mechi tisa. Nao wachezaji wa kikosi cha Shallom Yassets baada ya kuingia dimbani mara 12 wamezoa alama 25 ambapo wamo kileleni.

Kocha huyo anasema ana tajriba ya miaka nyingi ambapo anapania kuongoza kikosi hicho kuhakikisha kinapandishwa ngazi kushiriki ngarambe ya juu nchini.

Kadhalika anadokeza kuwa wanataka kujikaza kisabuni angalau watinge levo ya kushiriki soka la Ligi Kuu ya KPL. ”Itakuwa furaha kubwa kwa wafuasi wa Re-Union endapo itafaulu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya KPL,” alisema na kuongeza kwamba anatoa mwito kwa wafadhili wajitokeze kuwapiga jeki kwenye juhudi za kupaisha soka la kikosi hicho.

Mapema mwaka huu Re Union ilisajili wachezaji kadhaa wapya wakiwamo Brian Ochieng, kiungo mkabaji George Omondi na Kevin Odhiambo wote (Kanyaboli FC), Oscar Ochieng, stopa Wycliffe Onyango, Moses Okaro na Maurice Brian wa Alego Usonga FC na Malanga Combined mtawalia. Pia wapo, Felix Ochieng na Nehemia Omondi.

Klabu hii inajivunia kulea wachana nyavu wengi tu hapa nchini kama: Jacob Kelly, Eric Masika, Ochieng Era na Joseph Shikokoti kati ya wengine. Re Union inajivunia kuibuka ya kwanza kubeba taji la Afrika Mashariki na Kati mara mbili mwaka 1976 na 1977. Kadhalika iliwahi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu nchini mara mbili mwaka 1964 na 1975.

You can share this post!

ANNETTE MUCHITI: Filamu ina raha lakini changamoto zipo

Kangemi Ladies kusajili wachezaji sita

adminleo