Michezo

Wakenya walemewa kwenye mbio za Hamburg

April 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA waliendelea kuona vimulimuli katika mbio za kilomita 42 za Hamburg nchini Ujerumani baada ya wakimbiaji wake bora Solomon Yego na Sylvia Kibet kumaliza katika nafasi ya nne Aprili 29, 2018.

Yego alitumia saa 2:07:37 kukamilisha katika nafasi ya nne, huku Wakenya wenzake Vincent Kipruto (2:10:31), Stephen Chebogut (2:10:33) na Emmanuel Mutai (2:11:57) wakiridhika katika nafasi za sita, saba na tisa, mtawalia.

Mutai, ambaye muda wa wa saa 2:03:13 ni wa nne bora katika marathon nyuma ya mshikilizi wa rekodi ya dunia Dennis Kimetto (2:02:57), Muethiopia Kenenisa Bekele (2:03:03) na bingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge (2:03:05), alikuwa amepigiwa upatu sana wa kuibuka mshindi.

Hata hivyo, Ethiopia ilifagia nafasi tatu za kwanza kupitia Solomon Deksisa (2:06:34), Tadu Abate (2:06:54) na Ayele Abshero (2:07:19).

Katika kitengo cha wanawake, Kibet na Selly Chepyego ndiyo Wakenya pekee waliomaliza ndani ya mduara wa 10-bora.

Kibet alikamilisha katika nafasi ya nne kwa saa 2:30:27 naye Chepyego akaridhika katika nafasi ya nane (2:38:16). Mbahraini Shitaye Eshete, ambaye ni mzawa wa Ethiopia alinyakua taji kwa saa 2:24:51. Alifuatwa na Waethiopia Birke Debele (2:25:28) na Mimi Belete (2:26:06), mtawalia.