Blatter matatani kwa kukopa Sh100 milioni FIFA
Na CHRIS ADUNGO
RAIS wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Sepp Blatter anachunguzwa kwa matumizi mabaya ya mkopo wa Sh100 milioni ambao FIFA unadaiwa kutoa kwa Shirikisho la Soka la Trinidad & Tobago mnamo 2010.
Kwa mujibu wa stakabadhi rasmi za kisheria zilizowasilishwa mahakamani na waendeshaji mashtaka nchini Uswisi, Blatter ni ‘mshtakiwa’.
Madai hayo ndiyo ya hivi karibuni zaidi dhidi ya Blatter kuhusiana na ufujaji wa fedha akiwa kiongozi wa FIFA.
Ingawa hivyo, kinara huyo mwenye umri wa miaka 84 amekana kuwahi kufanya makosa yoyote akiwa uongozini.
Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa kortini, mkopo wa Sh100 milioni ambao haukuwa ulipwe na riba yoyote ulitolewa kwenye mojawapo ya akaunti za benki za FIFA bila udhamini wowote mnamo Aprili 13, 2010. Stakabadhi zinadai kuwa malipo ya mkopo huo yalifutiliwa mbali pindi baadaye kwa kuwa aliyekopeshwa alishindwa kurejesha fedha hizo.
Katibu Mkuu wa zamani wa FIFA, Jerome Valcke na Mkurugenzi wa masuala ya fedha wa FIFA Markus Kattner pia ni washtakiwa katika kesi hiyo.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendeshwa na Thomas Hildbrand aliyejiunga na FIFA mwaka wa 2019 kwa nia ya kufanikisha upelelezi na kufichua uozo uliowahi kufanyika katika shirikisho hilo katika miaka ya awali ili watuhumiwa wachukuliwe hatua kali za kisheria.