Michezo

Ndoa za wachezaji wa Chemelil Sugar zavunjika

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Charles Odera wa Chemelil Sugar amesema ndoa za wanasoka wao wanne zimevunjika huku wengi wakifurushwa kwenye nyumba walizokuwa wakiishi kutokana na athari za janga la corona.

Kwa mujibu wa Odera, uchechefu wa fedha unaoshuhudiwa na wachezaji wa Chemelil umewanyima fursa za kukimu mahitaji ya kimsingi za familia zao pamoja na kulipa kodi za nyumba kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.

“Wanasoka wanne wametorokwa na wake zao na baadhi wameachana na wachumba wao baada ya mifuko ya fedha kukauka. Ipo idadi kubwa ya wachezaji ambao wamefungiwa nyumba na wakaamua kuishi na marafiki zao au kurejea kwao mashambani,” akasema Odera kwa kusisitiza kuwa baadhi ya wachezaji wamelazimika kujishughulisha na kazi za sulubu na vibarua vya kila sampuli vya kijungujiko.

Odera kwa sasa amewataka wanasoka wa vikosi mbalimbali za soka ya humu nchini kutumia vyema mapato yao baada ya ukawaida wa hali kurejea na kuwekeza zaidi katika masomo yatakayowapa fursa mbadala za utaalamu utakaowafungulia milango zaidi ya ajira.

“Wapo wachezaji ambao wamelazimika kufanya kazi za ujenzi ili kujitafutia riziki ya kuendesha familia zao. Hivi ndivyo corona imeshusha kabisa soka yetu. Hata hivyo, naamini kuwa wengi wamepata mafunzo mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuwekeza na haja ya kurejea shuleni,” akasema.

Serikali tayari inatoa Sh10,000 kila mwezi kwa kila mchezaji wa vikosi 12 vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) isipokuwa Bandari FC, Tusker, Posta Rangers, Wazito, wanabenki wa KCB na wanajeshi wa Ulinzi Stars.