Kenya yapaa katika viwango vya ubora wa vikapu Afrika
Na CHRIS ADUNGO
KENYA imepanda hadi nafasi ya tatu barani Afrika kwa mujibu wa orodha mpya ya viwango vya ubora ya Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Vikapu (FIBA).
Misri wanashikilia nafasi ya kwanza kwa pointi 242 huku Mali wakiwa wa pili kwa alama 155. Pointi 122 za Kenya zinawaweka katika nafasi ya tatu mbele ya Nigeria, Uganda, Togo, Senegal, Madagascar, DR Congo na Algeria kwenye orodha ya timu 10-bora za Afrika.
Kwa mujibu wa Hilmi Ali ambaye ni mwenyekiti wa Shirikisho la Mchezo wa Vikapu nchini Kenya (KBF), kupaa kwao kwa nafasi tatu zaidi ni zao la juhudi za washikadau wote wakiwemo wachezaji ambao wamejituma katika kila mchuano na viongozi ambao wamepania kuchangia makuzi ya vipaji na maendeleo ya mchezo huo humu nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kikubwa zaidi ambacho Ali anaamini kilizolea Kenya pointi tele kwenye orodha mpya ya FIBA, ni ufanisi wa KBF kuandaa jumla ya mapambano 13 tofauti katika msimu wa 2019-20.
“Mbali na kushiriki kampeni za kuwania ufalme wa bara la Afrika mwaka jana, tuliandaa michuano mingi ya ndani kwa ndani iliyotupa pointi nyingi zilizotupaisha zaidi,” akasema Ali.
Martin Buluma wa Chuo Kikuu cha Strathmore na Christine Akinyi wa Chuo Kikuu cha Zetech ndio wanaotawala orodha ya wanavikapu bora zaidi humu nchini.
Ali amekiri kwamba vikosi vimeanza mchakato wa kujiandaa kwa kampeni za msimu ujao wa 2020-21 na tayari timu sita kati ya 60 zikatakazonogesha mchezo wa vikapu katika kiwango cha madaraja tofauti zimewasilisha orodha ya wachezaji wao kwa KBF.