• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 2:56 PM
‘Uuzaji wa mboga za kienyeji unalipa’

‘Uuzaji wa mboga za kienyeji unalipa’

Na SAMMY WAWERU

Ni majira ya asubuhi, tunakutana na Ann Kinuthia akiwa katika harakati za kusukuma gurudumu la maisha ili kukithi mahitaji ya familia yake.

Ann ni mama wa watoto wawili, na isemwavyo kazi si kuzaa ila ni kulea, lazima ajikaze kisabuni kuwekelea tonge la mlo mezani.

Katika mradi wa kilimo cha mboga wa Clayworks, Mwiki Nairobi, huraukia alfajiri na mapema kuwahi mazao.

“Leo nimechelewa kuwasili. Hufika kati ya saa kumi na mbili na saa mbili asubuhi, sawa na wateja wengine kununua mboga ili kuuza sokoni,” Ann akaambia Taifa Leo Dijitali wakati wa mahojiano katika mradi huo.

Ni mnunuzi jumla wa mboga za kienyeji, ili kuuzia walaji katika masoko mbalimbali Kiambu na Nairobi. Amekumbatia uuzaji wa mboga kama vile terere maarufu kama mchicha, sucha pia managu (mnavu), kunde na kansara (Ethiopina kales).

Mama huyu pia huuza mboga aina ya mito na murenda, na kimsingi mboga asilia za kienyeji zinashuhudia ushindani mkali sokoni  kutokana na uwezo wake kuongeza kinga mwilini, hasa wakati huu kila mmoja anachukua tahadhari dhidi ya kuambukizwa ugonjwa wa Covid – 19.

Baada ya kutayarishia familia yake kiamsha kinywa ikizingatiwa kuwa shule zimefungwa, ratiba yake kuzimbua riziki hung’oa nanga katika eneo la Clayworks.

Anasema aliingilia uuzaji wa mboga mwishoni mwa Machi 2020, siku chache baada ya kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona kuripotiwa nchini. Aidha, Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa Covid – 19 mnamo Machi 13, na visa vya maambukizi vinaendelea kuongezeka kila uchao.

Mama huyu anadokeza kwamba alikuwa mfanyakazi katika kampuni ya Coca Cola, ambapo alijukumika kusambaza vinywaji katika hafla au sherehe. “Tulikuwa tukisafiri sehemu mbalimbali nchini kusambaza vinywaji vya kampuni ya Coca Cola, hususan katika hafla,” anasema.

Ann akinunua mboga za kienyeji katika mradi wa kilimo cha mboga Clayworks, Mwiki, Nairobi. Picha/ SAMMY WAWERU.

Ilikuwa kazi yenye mapato ya kuridhisha, na anayosema alikuwa ameifanya kwa muda wa miaka minane mfululizo.

Hata hivyo jinamizi la Covid – 19 na ambalo ni janga la kimataifa lilimsimaisha ajira ghafla pamoja na wafanyakazi wenza. Janga la corona limeyumbisha uchumi wa mataifa mengi ulimwenguni, ikiwemo kuathiri sekta zote.

Baadhi ya biashara na kampuni zimefungwa, hatua ambayo imesababisha watu kupoteza nafasi za kazi.

Huku visa vya maambukizi vikiendelea kuongezeka, Ann anasema alianza kuhisi athari za ugonjwa wa corona mwishoni mwa mwezi Machi na kwa kuwa lazima maisha yangesonga mbele, hakuwa na budi ila kuingilia biashara ya uuzaji wa mboga za kienyeji.

“Baada ya kufanya hesabu, niliona biashara ya bidhaa za kula ndiyo bora kipindi hiki kwa sababu lazima watu wale,” anaeleza.

Isitoshe,anaeleza kwamba chaguo la mboga za kienyeji analisifia akisema halijamuangusha. “Mboga ni kitoweo ambacho huliwa kila siku katika maboma ya familia nyingi nchini. Chaguo la mboga za kienyeji ni bora, watu wakizikumbatia ili kuimarisha kinga ya mwili,” anafafanua, kauli inayopigwa jeki na Brian Nyongesa ambaye ni mkulima.

Ann Kinuthia, baada ya kupoteza ajira katika kampuni ya Coca Cola aliingilia uuzaji jumla wa mboga za kienyeji ambazo soko lake limenoga

Kulingana na Brian, mwenye uzoefu wa miaka kadhaa kukuza mboga za kienyeji, “Ikiwa kuna wakati soko la mboga asilia limenoga, uite baada Kenya kuthibitisha kuwa mwenyeji wa virusi vya corona. Wengi wanazila ili kuimarisha kinga ya mwili.”

Mboga za kienyeji zinasifiwa kwa kusheheni madini tofauti na pia kutokuwa na asidi, hasa kwa wenye matatizo ya asidi tumboni. Tija hizo kiafya, Brian anasema zimechangia soko la mboga za kienyeji kunoga. “Kwa mfano, mito, murenda, kunde, terere na managu ni mithili ya mahamri moto sokoni,” mkulima huyo anaeleza.

Hata ingawa mapato ni ya chini akilinganisha na kazi aliyokuwa akifanya awali, wakati wa mahojiano Ann alisema kwa siku akiondoa gharama ya matumizi hakosi kutia kibindoni faida ya Sh800.

Shirika la Afya Duniani limeonya kuwa janga la Covid – 19 huenda likakawia kudhibitiwa, ikikumbukwa kwamba chanjo na tiba haijapatikana. Kufuatia tahadhari hiyo, Ann anasema shabaha yake pia ni mkulima wa mboga za kienyeji.

You can share this post!

Arsenal yaadhibiwa 3-0 Luiz akila kadi nyekundu

Mtoto afariki katika kisa cha moto Mukuru-Kayaba

adminleo