Serikali yakiri corona inachangia mimba za mapema
Na JUMA NAMLOLA
SERIKALI inafuatilia kwa karibu ripoti kuhusu mimba za mapema miongoni mwa watoto wa kike.
Waziri msaidizi wa Wizara ya Afya, Dkt Mercy Mwangangi alisema kuendelea kuwepo kwa kanuni za kudhibiti virusi vya corona kunaathiri wananchi, ikiwemo ongezeko la mimba za mapema.
“Ijapokuwa kanuni zimetusaidia kukabili maambukizi ya corona, zimechangia maovu katika jamii kama vile mizozo ya kinyumbani na mimba za mapema,” akasema.
Dkt Mwangangi alikiri kuwa mimba kwa watoto wadogo ni changamoto kubwa kwa nchi, hali inayofaa kukabilia na wadau wote.
Wiki jana, kulisambazwa mitandaoni orodha zilizodai kuwa katika Kaunti ya Machakos, watoto wa kike 4,000 walitungwa mimba tangu masomo yalipositishwa Machi.
Ingawa huenda takwimu hizo zikawa si za kweli, visa vya uja uzito kwa wanafunzi vimekuwepo karibu kila mwaka.
Alikuwa akizungumza wakati wa kutoa taarifa kuhusu hali ya maambukizi, ambapo alitangaza watu 155 zaidi waliambukizwa katika saa 24.
Nairobi iliongoza kwa visa 104 ikifuatwa na Busia (19), Migori (10), Mombasa (9) na Uasin Gishu (4). Kaunti nyingine zilikuwa Kiambu (3), Machakos (2), Nakuru (2), Kisumu (1) na Kajiado (1).
Jana pia wagonjwa 102 waliruhusiwa kwenda nyumbani na kufikisha idadi ya waliopona kutokana na Covid-19 kuwa watu 1,782. Serikali ilisema inashirikiana na Baraza la Magavana (CoG) kuhakikisha kuwa vifaa vya kupimia watu vilivyosambazwa ni vya hali inayokubaliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).