• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Fainali ya Chapa Dimba kukosa uhondo kisa corona

Fainali ya Chapa Dimba kukosa uhondo kisa corona

Na JOHN KIMWERE 

IDADI ya waathiriwa wa ugonjwa wa Covid-19 inazidi kuongezeka hapa nchini hali inayoendelea kuzima mpango wa kufungua shughuli nyingi ikiwamo michezo. 

Wadau wa michezo na wananchi kwa jumla wamejikuta njiapanda baada ya rais Uhuru Kenyatta kuongoza muda wa marufuku ya mikusanyiko ya umma hadi mapema mwezi ujao.

Wadau wa spoti hapa chini  bila kuweka katika kaburi la sahau vikosi vya mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three wana kiu cha kurejea dimbani kukamilisha fainali za Mikoa kisha fainali za kitaifa.

Fainali za makala ya muhula huu zilikuwa ziandaliwa wikendi ya juma lililopita katika Kaunti ya Mombasa lakini kwa sasa hali si hali tena.

FALLING WATERS

Ofisa wa kitengo cha habari za michuano hiyo, Steve Kanja amesema “Kiukweli mkurupuko wa virusi vya corona vinavyochangia ugonjwa wa Covid-19 umesitisha shughuli za mashindano ya msimu huu lakini tunalenga kurejea baada ya hali kudhibitiwa.”

Kampeni za mashindano hayo zilipigwa breki mwezi Machi kufuatia mlipuko huo huku ikiwa zimesalia fainali za mikoa mwili: Mkoa wa Magharibi na Nyanza.

Michuano hiyo ilisitishwa huku fainali za mikoa sita zikiwa zimechezwa na washindi kupatikana waliojikatia tiketi za kushiriki fainali za kitaifa.

Kocha wa timu ya wasichana ya Falling Waters mabingwa wa Mkoa wa Kati, Emma ‘Gullit’ Wambuchi anasema ”Vigoli wangu walikuwa na hamu kubwa kuonyesha uwezo wao katika fainali za kitaifa lakini janga la ugonjwa wa Covid-19 kiasi limezuia matamanio hayo.”

Timu hiyo ambayo awali ilifahamika kama Barcelona Ladies ilitwaa tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa ilipobugiza Limuru Starlets kwa magoli 3-1. Kikosi hicho kitashiriki fainali za kitaifa kwa mara ya pili baada ya kuwakilisha mkoa huo katika kipute cha msimu uliyopita.

WIYETA GIRLS

Kocha huyo alidokeza kuwa hali ya sasa huenda ikabomoa ubora wa wachezaji wao baada ya kukaa bila kushiriki mazoezi ya pamoja kwa muda mrefu. Kadhalika alisema kuwa wachezaji wote walikuwa wamejipanga kiume kuelekea fainali za muhula huu lakini janga linaotesa dunia nzima tayari zimewavunja moyo.

”’Licha ya mashindano hayo kusitishwa bado tunatarajia kushusha ushindani mkali kupigania ubingwa wa taji la kitaifa,” nahodha wa Falling Waters, Miriam Lutomia alisema na kuongeza kuwa huenda fainali hizo zikakosa uhondo kama ilivyotarajiwa kabla ya kuzuka kwa mkurupuko wa Covid-19.

Baada kukosa tiketi ya fainali ya kipute hicho mwaka uliyopita, Wiyeta Girls ya Mkoa wa Bonde la Ufa ilifuzu kwa fainali za msimu huu ilichoma Itigo Girls kwa mabao 3-0.

Orodha ya timu zingine zilizofuzu kushiriki fainali za kitaifa  inajumuisha: Beijing Raiders (Mkoa wa Nairobi), Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.

You can share this post!

Kibera Utd, Ruiru Hotstars kusaka ubabe Daraja la Pili

SUSAN KING’ORI: Napenda kufanya kazi na Maria wa...

adminleo