• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
AKILIMALI: Ukuzaji nyanya utakuletea malaki ya hela

AKILIMALI: Ukuzaji nyanya utakuletea malaki ya hela

Na JOHN NJOROGE

[email protected]

Sio wakulima wengi wanaoamini kuwa kukuza mimea kupitia mahali kuna kivuli hunawiri na kutoa mazao ya kufaa.

Lakini Bi Margaret Nyambura Njuguna anaamini kuwa kupanda mimea kwa nyumba ya kioo (greenhouse) ndio mojawapo ya njia ambazo mkulima mdogo anayekuza nyanya ama mimea ingine ya muda mfupi anafaa kutumia.

Akivalia aproni ya kahawia, viatu vyeusi vilivyo wazi na vazi ndefu la madoadoa, Bi Njuguna anaangalia nyanya zake zilizoiva ndani ya chumba chake cha vioo katika shamba la Turi, kilomita mbili kutoka mji wa Elburgon katika kaunti ya Nakuru.

Bi Njuguna alianzisha chumba hiki cha mita sita kwa nane mwaka wa 2018 na kutumia shilingi elfu arobaini (40,000) katika matumizi ya ujenzi, mbolea na mbegu za kupanda.

“Nilitumia miche 450 ambazo ziliidhinishwa na huduma ya ukaguzi wa mimea nchini (Kephis) kwa dhamana ya shilingi elfu tatu (3,000),’’ akasema Bi Njuguna, akiongeza kuwa alitenganisha miche yake ya Anna F-1 aliyoipanda kwa nafasi ya 45cm kwa 60cm.

Akiongea na Akili Mali hivi majuzi, Bi Njuguna alisema kuwa alipanda nyanya zake kwa umbali wa hatua moja ili kuziwezesha kupata nafasi nzuri ya kukua.

Mkulima huyu alikiri kuwa kukuza nyanya katika chumba cha vioo husaidia kwa hali ya kiuchumi na pia kukinga mimea kutoka kwa jua kali na mvua kubwa inaponyesha.

“Kwa kutumia maji ya dondosha, nyanya huongeza mazao kwa kupokea joto inayofaa,’’ akasema, akiongeza kuwa ndani ya chumba hiki, nuru ya jua na maji ya mvua ya kiwango cha chini ndio huhitajika.

Mkulima huyu ambaye pia ni mmiliki wa duka la Millenium Agro-Vet mjini Elburgon, alisema kuwa kabla nyanya zake zilizochukua miezi minne kukua, alinyunyizia dawa ili kuua wadudu weupe wanaovamia matawi ya nyanya.

Katika mwaka wa 2018, alikumbuka vile mapato yake ya nyanya yalififia kwa vile hakunyunyizia dawa ya wadudu kwa wakati unaofaa.

“Katika mwaka huo ambao ndio ulikuwa wangu wa kwanza kupanda nyanya kwa kutumia nyumba ya vioo, nilipata hasara zaidi ya shilingi elfu ishirini (20,000) kwa kutonyunyizia dawa kwa wakati ufaao. Hasara hiyo ilikuwa ni baadhi ya pesa za mbegu na kazi ya shamba niliyotumia,’’ akasema mkulima huyu, akiongeza kuwa wadudu hao weupe huvamia mimea hasa wakati wa baridi ambapo mkulima hushauriwa kunyunyizia dawa kila mwezi.

Alisema ingawa kulika virusi vya Covid-19 Machi mwaka huu, hakuathirika sana kwa vile mauzo yake alikuwa akiiuza kwa soko la ndani.

“Mauzo yangu imeongezeka tangu ugonjwa huu wa Corona ulipofika nchini. Wafanyibiashara wa ndani ambao walisafiri sehemu zingine za nchi kutafuta nyanya wameamua kuzinunua huku, na walioenda kuuza kwa soko za nje, wanaziuza hapa pia,’’ akasema.

Bi Njuguna alisema kwa siku nzuri, yeye huuza kreti moja ya nyanya kwa shilingi elfu tau (3,000) na shilingi elfu moja mia tano (1,500) wakati nyanya ni nyingi sokoni mtawalia.

Bi Njuguna anayevuna mara mbili kwa wiki, akitabasamu alisema kuwa yeye hupata kati ya shilingi elfu tano (5,000) na shilingi elfu sita (6,000) kwa wiki moja katika sehemu yake ndogo aliyoipanda nyanya.

Kwa muda wa miaka mitatu mfululizo ambayo alizipanda nyanya, Bi Njuguna anakumbuka vile alipata shilingi elfu sabini (70,000), pesa nyingi ambazo aliwahizipata tangu mwaka wa 2018 alipoanza kupanda Anna F-1.

“Kwa wakati huo, mahitaji ilikuwa juu kwa vile wakulima wachache ndio walipanda nyanya kwa mwaka huo. Nilivuna mara mbili kwa wiki na kupata shilingi elfu tano (5,000) kwa kila kreti niliyouza,’’ akasema.

Alikiri kuwa mbali na sehemu ndogo aliyoipanda nyanya zake, amepata pesa nyingi ambazo hakutarajia kutoka kwa sehemu hiyo. Bi Njuguna ana mpango wa kupanda nyanya zaidi kwa ekari mbili za shamba baada ya kupata mapato mazuri kwa miaka mitatu iliyopita.

Afisa wa kilimo katika kaunti ndogo ya Molo Bw Alfred Waithaka amewaomba wakulima kufuata maagizo yanayofaa wakati wa kunyinyizia mimea yao.

Waithaka alisema kuwa mdudu Tuta Absoluta ambaye huvamia matawi na shina ya mimea, anafaa kunyunyiziwa dawa ya Coragen mara kwa mara inayomuua kwa upesi.

Aliongeza kuwa kwa kuchoma Sulphur, wadudu hao hufa wakati mawimbi ya moshi inapowapata ndani ya nyumba hiyo ya vioo.

Alisema mmea wa nyanya hudidimia na kupunguza mazao wakati inaponyunyiziwa dawa vibaya na kwa wakati ambao haufai. Waithaka alisema Late Bright ni ugonjwa unaovamia nyanya kwa haraka na kuangamiza mmea kwa jumla na pia kuenea kwa mimea nyingine.

“Mdudu huyu ana uharibifu mkubwa na wakulima huombwa kunyunyizia dawa mara mbili kwa mwezi,’’ akasema Waithaka na kuongeza kuwa virusi vya Mosaic huvamia matunda hayo pia.

Afisa huyo amewaomba wakulima kuzoea na kujifunza kupanda mimea ya mzunguko na kuandaa kalenda ya mzunguko ili kuepuka na mimea ya familia moja ambayo haifai kupandwa kwa wakati mmoja ama kwa mfululizo.

“Upanzi wa mimea ya familia moja kama vile viazi na kapu, husababisha maambukizi zaidi yaliyovamia mimea iliyopandwa awali kwa shamba moja,’’ akasema Waithaka.

Akiongea na Akili Mali, Waithaka alisema aina nyingi za nyanya hukomaa kati ya miezi mitatu na miezi mitatu unusu. Aliongeza kuwa zao hili linawezavunwa hadi muda wa mwaka mmoja iwapo limeshughulikiwa vizuri.

Bwana Waithaka alisema kuwa changamoto kubwa kwa wakulima ni soko lakini aliwaomba kujaribu aina tofauti za nyanya ilikubainisha ni ipi ingefaa kwa sehemu fulani kwa wakati tofauti.

You can share this post!

EVELYN MUKIRI: Nitarejea kwa kishindo katika majukwaa ya...

Mafuriko yalivyowaletea wakulima wa mahindi hasara

adminleo