Werner kujiunga na Chelsea mwishoni mwa msimu
Na CHRIS ADUNGO
CHELSEA wamethibitisha kwamba fowadi Timo Werner, 24, atajiunga nao rasmi mwishoni mwa muhula huu baada ya kuagana na RB Leipzig kwa kima cha Sh7.4 bilioni.
Werner ambaye kwa sasa amefungia timu ya taifa ya Ujerumani mabao 11 kutokana na mechi 29 zilizopita, alitia saini mkataba wa miaka minne utakaomshuhudia akitia kapuni kima cha Sh24 milioni kwa wiki na Sh1.3 bilioni kwa mwaka.
Ujio wa Werner utamfanya kuwa sogora anayedumishwa kwa mshahara mnono zaidi uwanjani Stamford Bridge mbele ya Kepa Arrizabalaga, N’Golo Kante, Christian Pulisic, William na Callum Hudson-Odoi. Wanasoka wengine wanaopokezwa kitita kinono zaidi cha fedha kambini mwa Chelsea ni Jorgino, Olivier Giroud, Mateo Kovacic, Ross Barkley na Pedro Rodriguez.
Kocha Frank Lampard amefichua kwamba alifunga safari ya kuelekea Ujerumani kwa kipindi cha siku nne kufanikisha mipango ya kumsajili Werner mnamo Januari 2020 kabla ya kulipuka kwa janga la corona.
Hata baada ya kuripotiwa kwa visa vya maambukizi ya corona nchini Uingereza, Lampard amesisitiza kwamba aliendelea kuwania maarifa ya mshambuliaji huyo kupitia mawasiliano ya mara kwa mara ya simu.
Werner ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Stuttgart, anabanduka kambini mwa Leipzig baada ya kipindi cha misimu minne iliyomshuhudia akipachika wavuni jumla ya mabao 93 kutokana na mechi 157.
Hadi kufikia sasa, Werner anajivunia kuwafungia Leipzig jumla ya mabao 32 na kuchangia mengine 13 kutokana na mechi 43 zilizopita ambazo amewajibishwa katika mapambano yote.
Sogora huyo anatarajiwa kutua ugani Stamford Bridge baada ya mechi mbili zilizosalia katika kampeni za Ligi Kuu ya Ujermani (Bundesliga) msimu huu kusakatwa.
Waajiri wake wanahitaji alama mbili pekee kutokana na mechi hizo dhidi ya Borussia Dortmund na Augsburg ili kujipa uhakika wa kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao. Leipzig wamo katika robo-fainali za UEFA msimu huu baada ya kuwabandua Tottenham Hotspur kwenye hatua ya 16-bora.
Werner hatakuwa sehemu ya kampeni za Chelsea msimu huu kwenye mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya UEFA dhidi ya Bayern Munich uwanjani Allianz Arena, Ujerumani.
Kipute cha UEFA msimu huu kinatazamiwa kutamatika rasmi mnamo Agosti 2020 huku mechi zilizosalia zikiandaliwa Lisbon, Ureno. Jiji la Lisbon liliwahi kuwa mwenyeji wa fainali ya UEFA kati ya Real Madrid na Atletico Madrid mnamo 2014.
Werner huenda akajumuika na mchezaji mwenzake wa Leipzig, Kai Havertz uwanjani Stamford Bridge iwapo Chelsea watafaulu kumshawishi kubanduka kambini mwa Bayer Leverkusen.