Michezo

Hatutasajili mchezaji mpya – Kariobangi Sharks

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KARIOBANGI Sharks hawatasajili mwanasoka yeyote katika muhula ujao wa uhamisho wa wachezaji kwa minajili ya kampeni za msimu wa 2020-21 katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Haya ni kwa mujibu wa mwenyekiti wao, Robert Maoga ambaye amethibitisha kwamba mabingwa hao wa zamani wa Shield Cup badala yake watawaachilia angalau masogora watano ambao usimamizi umehisi kuwa huduma zao hazihitajiki kwa sasa.

Maoga amesema kwamba maamuzi hayo yamechukuliwa na Sharks kutokana na ukubwa wa gharama ya kuwadumisha wanasoka wao kimshahara hasa wakati huu ambapo hazina yao ya kifedha imelemazwa na ugonjwa wa Covid-19.

Kulingana naye, watakaokosekana kwenye mpango wa baadaye wa kikosi watakuwa na fursa ya kusaka hifadhi mpya kwingineko hata kabla ya muhula wa uhamisho wa wachezaji kufunguliwa rasmi.

Maoga amesisitiza kwamba Sharks wanapania kusalia na wachezaji 25 pekee kikosini mwao kuliko idadi kubwa ya sasa. Aidha, amefichua kwamba wachezaji watakaoagana nao wamefahamishwa kuhusu hatima yao na wataendelea kulipwa mishahara hadi janga la corona litakapodhibitiwa na soka ya humu nchini kurejelewa.

“Tuna zaidi ya wachezaji 30 kwa sasa na hatuoni haja ya kuleta wanasoka wapya. Tumetambua wale ambao hawamo katika mipango yetu ya baadaye na tutawaachilia. Kuwa na kikosi cha wachezaji wachache hupunguza gharama ya matumizi na kuinua viwango vya ushindani,” akasema Maoga.

Wakati uo huo, Sharks wamesisitiza kwamba Yanga SC kutoka Tanzania wamewawasilishia maombi ya kutaka kusajili wafumaji Sven Yidah na Harrison Mwendwa. Wawili hao walikuwa tegemeo kubwa la Sharks kwenye fainali za SportPesa Super Cup mnamo Januari 2019.