Leno kukosa mechi zote za Arsenal
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI Neal Maupay aliyezamisha chombo cha Arsenal katika ushindi wa 2-1 waliousajili katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 23 amesema wapinzani wao walipata walichokitaka baada ya kumkashifu mno kwa jeraha alilolipata kipa Bernd Leno.
Leno alipata jeraha baya la goti na kifundo cha mguu baada ya kuanguka vibaya alipokuwa akiwania mpira wa juu kutoka kwa Maupay pembeni mwa kijisanduku.
Akiondolewa uwanjani kwa machela, Leno aliinuka na kuanza kumzomea Maupay na kumuotea kidole katika tukio lililoashiria ukubwa wa kiwango cha kufadhaishwa kwake na fowadi huyo mzawa wa Ufaransa.
Nafasi ya Leno ilijazwa na kipa Emiliano Martinez kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza wakati ambao vikosi vyote viwili vilikuwa vikitoshana nguvu kwa sare tasa.
Mwishoni mwa kipindi cha pili, Maupay alizingirwa tena na wachezaji wa Arsenal walioonekana kumsukuma kwa kumbo na kumgombeza kwa tukio lililochangia kuumia kwa Leno na hatimaye kushindwa kwao.
“Baadhi ya wanasoka wa Arsenal wanastahili kujifunza unyenyekevu,” akasema Maupay.
Kwa wakati fulani, kiungo Matteo Guendouzi ambaye pia ni mzawa wa Ufaransa alijipata akivutwa na wenzake kutoka kwa Maupay baada ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.
Guendouzi alikuwa akipania kuzua kizaazaa na kutishia kumrukia na kumkabili Maupay baada ya wawili hao kuonekana wakikaripiana walipokuwa wakiondoka uwanjani.
“Mmoja wao alikuwa akiongea sana kipindi kizima cha mchezo na kurusha cheche za matusi ya kila sampuli,” akasema Maupay.
“Nilipofunga, nilijisema ‘sikia, hili ndilo hufanyika wachezaji wa kikosi pinzani wanapotema matusi uwanjani.”
“Wakati wa mapumziko, nilimwendea kocha Arteta na kuomba msamaha. Sikukusudia kumjeruhi Leno. Niliruka tu kuwania mpira wa juu. Naomba msamaha kwa kikosi kizima na kipa Leno. Nimewahi kupitia hali hiyo na ninajua uchungu wa kupata jeraha,” akasema Maupay.
“Niliendea tu mpira kwa hakika. Leno alianguka vibaya na kuumia goti. Huu ni mpira wa soka na kuna kukabiliana. Sikulenga kumjeruhi. Naomba msamaha kwa mara nyingine na namtakia afueni ya haraka,” akasema Maupay.
Mchuano huo ulikuwa wa pili kwa Arsenal kupoteza mfululizo tangu kurejelewa kwa EPL kwa gozi liilowashuhudia wakipepetwa 3-0 na Manchester City. Kiungo Granit Xhaka wa Uswisi na beki mzawa wa Uhispania, Pablo Mari walijeruhiwa katika mchuano huo.
Arsenal walikosa pia huduma za beki David Luiz aliyekuwa akitumikia marufuku baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Man-City kwa kosa la pili la kumkabili vibaya kiungo Riyad Mahrez visivyo.