Mashabiki Ufaransa kuruhusiwa uwanjani Julai
Na CHRIS ADUNGO
MASHABIKI nchini Ufaransa watakuwa na idhini ya kuingia uwanjani kuanzia Julai 11, 2020 baada ya serikali ya taifa hilo kuanza kulegeza baadhi ya masharti yaliyowekwa ili kudhibiti maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19.
Wachezaji wapatao 5,000 ndio watakaoruhusiwa kuingia uwanjani kutazama baadhi ya mechi moja kwa moja japo idadi hiyo huenda ikaongezwa polepole wakati wa kampeni za msimu ujao katika soka ya Ufaransa.
Ina maana kwamba fainali za kuwania ubingwa wa French Cup na League Cup msimu huu huenda zikatandazwa mbele ya takriban mashabiki 5,000 baada ya vipute hivyo kuahirishwa hadi siku mpya itakayotolewa baadaye mwishoni mwa Juni 2020.
Soka ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) na ile ya daraja la kwanza (Ligue 2) zilisitishwa kwa muda mnamo Machi 10, 2020 kabla ya msimu huu wa vipute hivyo kufutiliwa mbali mwishoni mwa Aprili 2020.
“Tathmini mpya itatolewa na mwongozo mwingine utakaolenga kulegeza masharti yaliyopo kufichuliwa chini ya wiki mbili zijazo. Ilivyo, tunapania kurejesha baadhi ya shughuli za michezo polepole kuanzia Juni 22 huku mashabiki 5,000 wakiruhusiwa kufikia viwanjani kushabiki timu zao kufikia katikati ya Julai. Idadi hiyo itaongezeka kufikia Agosti 2020,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Serikali ya Ufaransa.
Baada ya ligi ya soka nchini Ufaransa kufutiliwa mbali, Paris Saint-Germain (PSG) walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). Hadi kufutiliwa mbali kwa kipute cha Ligue 1 zikiwa zimesalia raundi 10, PSG walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 12 zaidi kuliko Olympique Marseille ambao wanakamata nafasi ya pili kwa pointi 56.
Pindi baada ya kutangazwa wafalme wa soka ya Ligue 1 kwa mara nyingine msimu huu, PSG walisema kwamba ushindi huo ni zawadi muhimu kwa maafisa wote wa afya ambao wamekuwa wakijishughulisha vilivyo katika vita vya kukabiliana na ugonjwa wa corona.
Mwenyekiti wa PSG, Nasser Al-Khelaifi alitambua pia ukubwa wa mchango na kujitolea kwa maafisa wa afya ambao wamejinyima mengi katika kipindi cha wiki nyingi zilizopita za kukabiliana na corona.
Huku PSG wakitawazwa mabingwa kutokana na wingi wa alama zao, Lorient nao walipokezwa ubingwa wa Ligi ya Daraja ya Kwanza (Ligue 2). Lorient walikuwa wakijivunia alama 54, moja pekee kuliko Lens ambao ni wa pili.
Vikosi hivyo viwili vilipandishwa daraja kujaza nafasi za Amiens na Toulouse ambao walishushwa ngazi kwenye kipute cha Ligue 1 japo wameanzisha mchakato wa kisheria kupinga maamuzi ya kuteremshwa kwao.
Olympique Lyon ambao walikuwa katika nafasi ya tano wiki moja kabla ya mchuano wa mwisho wa msimu huu, walirushwa hadi nafasi ya saba. Kikosi hicho pia kimekata rufaa dhidi ya maamuzi ambayo yaliafikiwa na serikali kwa ushirikiano na vinara wa soka ya Ufaransa.
Kwa mujibu wa Lyon, wao wana haki ya kufidiwa mabilioni ya fedha ambazo vingenevyo wangezitia mfukoni kwa kufuzu kushiriki kipute cha Europa League iwapo msimu ungekamilishwa jinsi ilivyotarajiwa.