Real kileleni La Liga
CHRIS ADUNGO
REAL Madrid walipaa hadi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kuwacharaza Real Sociedad 2-1 mnamo Juni 21, 2020.
Real kwa sasa wanajivunia alama sawa na Barcelona (65) waliolazimishiwa sare tasa na Sevilla uwanjani Ramon Sanchez-Pizjuan mnamo Juni 19. Licha ya Barcelona kujivunia idadi kubwa ya mabao ikilinganishwa na Real, masogora hao wa kocha Zinedine Zidane wanaorodheshwa juu ya Barcelona kutokana na ubora wa rekodi yao dhidi ya mabingwa hao watetezi wa La Liga.
Beki na nahodha Sergio Ramos aliwafungulia Real ukurasa wa mabao kunako dakika ya 50 kupitia penalti iliyotokana na tukio la fowadi Vinicius Jr kuchezewa vibaya na Diego Carlos ndani ya kijisanduku.
Karim Benzema aliwafungia Real bao la pili kunako dakika ya 70 kabla ya Mikel Merino kuwafutia Sociedad machozi mwishoni mwa kipindi cha pili.
Kuliibuka utata baada ya Adnan Januzaj kudhania alikuwa ameyafanya mambo kuwa 1-1 kabla ya juhudi zake kufutiliwa mbali na refa kwa madai kwamba alifunga Merino akiwa ameotea. Japo Merino hakubadilisha mwelekeo wa kombora la Januzaj, teknolojia ya video ya VAR ilibaini kwamba fowadi huyo alikuwa amemzuia kipa Thibaut Courtois.
Bao la Benzema lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Federico Valverde ambaye nusura awafungie Real bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili kutokana na krosi ya Roberto Lopez.
Pigo la pekee kwa Real ni jeraha la mguu lililomlazimisha Ramos kuondoka uwanjani pindi baada ya kuchanja mkwaju wa penalti.
Real ambao wamenyanyua ubingwa wa La Liga mara moja pekee tangu 2012, sasa wanahitaji kusajili ushindi katika mechi zote nane zilizosalia msimu huu ili kuwapiku washindani wao wa tangu jadi, Barcelona.
Chini ya kocha Quique Setien, Barcelona watakuwa wenyeji wa Athletic Bilbao uwanjani Nou Camp mnamo Juni 23 huku Real wakipangiwa kuvaana na Mallorca siku moja baadaye ugani Alfredo Di Stefano.
Katika mechi nyinginezo za Juni 23, Getafe watakabiliana na Valladolid nao Levante wapimane ubabe na Atletico Madrid ambao wana ulazima wa kusajili ushindi ili kuweka hai matumaini ya kunogesha kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.
MATOKEO YA LA LIGA (Juni 21):
Sociedad 1-2 Real Madrid
Celta Vigo 6-0 Alaves
Valencia 2-0 Osasuna