Michezo

Mane asahau kupiga goti debi ikianza

June 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

SADIO Mane wa Liverpool alikuwa na kiu kubwa ya kurejea kunogesha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kiasi kwamba alisahau kupiga goti kama walivyofanya wachezaji wenzake sekunde chache kabla ya kuanza kwa gozi lililowakutanisha na Everton.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi yoyote ya EPL kupulizwa tangu soka kurejelewa baada ya janga la corona, imekuwa desturi kwa wanasoka kupiga goti chini ili kuunga maandamano dhidi ya matukio ya ubaguzi wa rangi miongoni mwa wakazi wa Amerika na mataifa mengine ya bara Ulaya.

Bila kutarajia, Mane alijipata akikimbia kuelekea upande wa lango la Everton baada ya kocha Mike Dean kupuliza kipenga cha kuashiria wachezaji kupiga goti.

Baada ya kutambua kosa lake, fowadi huyo wa Senegal mwenye umri wa miaka 28 alirejea kwenye upande wao halahala na kupiga goti jinsi ilivyofanywa na wenzake na wanasoka wote wa Everton.

Wachezaji wa EPL wamekuwa wakipiga goti kulalamikia ubaguzi wa rangi tangu kuauwa kwa Mmarekani mweusi George Floyd katika kituo cha polisi jijini Minneapolis, Amerika.

Mwanasoka Colin Kaepernick wa Amerika ndiye mchezaji aliyeanza desturi ya kupiga goti kulalamikia suala la ubaguzi wa rangi nchini humo mnamo 2016. Mchezaji huyo wa Ligi ya NFL alikuwa akifanya hivyo kila mara wimbo wa taifa wa Amerika ulipokuwa ukiimbwa kabla ya mechi za kimataifa.

Wakati uo huo, Liverpool wameanza kuingiwa na hofu ya kupoteza huduma za Mane baada ya sogora huyo kukataa kutia saini mkataba mpya. Mane anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua kambini mwa Real Madrid ya Uhispania kwa kima cha Sh21 bilioni.

Kwa mujibu wa kocha Jurgen Klopp, majaribio yake ya mara kwa mara kwa kipindi cha miezi tisa iliyopita ya kumsadikisha Mane kurefusha muda wa kuhudumu kwake uwanjani Anfield hadi 2023 bado halijazalisha matunda yoyote.

Liverpool wanatarajiwa wiki hii kumpokeza beki Virgil van Dijk mkataba mpya wa thamani ya Sh35 bilioni utakaotamatika rasmi mnamo 2025.