Michezo

Sofapaka kusajili beki wa Rwanda

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

SOFAPAKA wamefichua kwamba wanakaribia kukamilisha mpango wa kumsajili beki matata mzawa wa Rwanda kwa minajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Japo Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) halijafungua rasmi muhula wa uhamisho wa wachezaji, Rais Elly Kalekwa wa Sofapaka amesema kikosi chake kimekuwa kikimvizia difenda huyo kwa kipindi kirefu na ni suala la muda tu kabla hajatua kambini mwao.

Hata hivyo, amekataa kufichua jina la mwanasoka huyo kwa hofu kwamba huenda wapinzani wao wakaanza kumnyemelea na kutumia ushawishi wao wa kifedha kumtwaa.

“Ni beki wa haiba kubwa ambaye atajiunga nasi bila ada yoyote kwa kuwa mkataba wake na waajiri wake wa sasa unakamilika mwishoni mwa mwezi huu. Tumeafikiana na wakala wake, yeye mwenyewe na familia yake inayofanya kazi humu nchini. Ilivyo, dalili zote zinaashiria kuwa atajiunga nasi,” akasema Kalekwa.

Sofapaka ambao walitawazwa mabingwa wa KPL mnamo 2009, wanasema wanalenga kujinasia huduma za wanasoka watano zaidi kwa ajili ya msimu mpya wa 2020-21.

Mbali na beki mzawa wa Rwanda, kikosi hicho kinapania kujitwalia huduma za beki wa zamani wa Gor Mahia, Musa Mohammed ambaye mkataba wake na mabingwa mara 12 wa Ligi Kuu ya Zambia, Nkana FC kutamatika mwanzoni mwa mwezi huu.

Musa alikuwa karibu kuingia katika sajili rasmi ya Sofapaka mnamo Aprili 2018 baada ya kuagana na kikosi cha FK Tirana nchini Albania.

“Tunaazimia kusajili wanasoka watano pekee ambapo watatu watakuwa raia wa kigeni. Tumetambua wachezaji hao tunaowalenga na mazungumzo ya kurasimisha uhamisho wao yameanza. Nina hakika kwamba Musa naye atajiunga nasi,” akasema Kalekwa.

Sofapaka tayari wameanzisha mchakato wa kisheria kuzuia uhamisho wa mvamizi John Avire ambaye kwa mujibu wa Kalekwa, aliyoyomea Misri mwishoni mwa 2019 kuvalia jezi za FC Tanta kinyume na kanuni za usajili zilizopo katika mwongozo wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).