Michezo

Arsenal yarefusha mkataba wa Luiz

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

BEKI David Luiz ametia saini mkataba mpya wa mwaka na Arsenal.

Mabeki Pablo Mari na Cedric Soares watajiunga pia na Arsenal kirasmi mwishoni mwa vipindi vyao vya mkopo uwanjani Emirates. Wawili hao wataachiliwa rasmi na klabu za Flamengo na Southampton kutoka nchini Brazil na Uingereza mtawalia.

Wakati uo huo, kiungo Dani Ceballos amerefusha kipindi chake cha mkopo kutoka Real Madrid kwa mwaka mmoja zaidi. Nyota huyo mzawa wa Uhispania sasa atasalia kuhudumu kambini mwa Arsenal hadi mwishoni mwa msimu 2020-21.

“Ni fahari kubwa kwamba tutasalia na wachezaji hawa wote kambini mwetu kwa minajili ya vibarua vijavyo,” akatanguliza Mkurugenzi wa Kiufundi wa Arsenal, Edu.

“Wanaleta nguvu mpya kikosini na kuwepo kwao kutainua viwango vya ushindani katika timu ambayo kwa sasa inasukwa upya na kocha Mikel Arteta,” akasema kinara huyo.

Luiz, 33, alijiunga na Arsenal mnamo 2019 baada ya kukatiza uhusiano wake na Chelsea. Hata hivyo, matokeo yake hayajakuwa ya kuridhisha uwanjani Emirates.

Alionyeshwa kadi nyekundu katika kichapo cha 3-0 ambacho Arsenal walipokezwa na Manchester City ligini mnamo Juni 17 baada ya masihara yake kuchangia bao la kwanza lililojazwa kimiani na Raheem Sterling katika gozi hilo la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mari, 26, ambaye ni beki wa kati mzawa wa Uhispania pia anauguza jeraha la mguu kwa sasa. Anatarajiwa kutia saini mkataba mpya kwa pamoja na Soares, 28, muhula wa uhamisho wa wachezaji utakapofunguliwa rasmi mwishoni mwa Julai 2020.