Makala

Wakenya wanaendelea kufurahia uhuru wa kutembea jioni baada ya saa za kafyu kutathminiwa upya

June 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KUTATHMINIWA upya kwa saa za kafyu ya kitaifa mnamo Juni 6, 2020 kulionekana kuleta afueni kwa wananchi wengi hasa wanaochelewa kutoka maeneo yao ya kazi.

Katika hotuba yake kwa taifa, Rais Uhuru Kenyatta alitathmini muda wa awali wa amri ya kutotoka nje usiku kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi na moja asubuhi, ukawa kati ya saa tatu usiku hadi saa kumi asubuhi.

Mabadiliko hayo yalijiri wakati ambapo Wakenya walikuwa na matumaini makuu kiongozi wa nchi angelegeza masharti na mikakati iliyowekwa kudhibiti usambaaji wa Covid- 19, wanayolalamikia yamechangia maisha kuwa magumu.

Huku maambukizi ya homa ya corona yakiripotiwa kuendelea kuongezeka kila uchao, tathmini ya saa za kafyu ilionekana kuleta afueni kwa wananchi.

Mabadiliko ya saa za kafyu yalianza kutekelezwa Juni 7, baadhi ya Wakenya wakieleza kuridhishwa nayo kwa kile wanataja kama ‘kuwarejeshea uhuru wa ratiba ya kawaida kufanya kazi’.

Utekelezaji wa kafyu ya kitaifa ulianza Machi 27, 2020, baada ya Kenya kuripoti kuwa mwenyej wa Covid – 19, kama njia mojawapo kusaidia kudhibiti maenezi zaidi.

“Hata ingawa kuna sekta ambazo hazijapata afueni, wengi wetu tunaridhia mabaliko ya saa za kafyu. Kwa sasa tunaweza kufanya kazi kama kawaida,” Nicholas Mwangi, ambaye ni mfanyabiashara jijini Nairobi ameambia Taifa Leo katika mahojiano.

Katika hotuba ya Rais Kenyatta, alisema mabadiliko ya saa za kafyu yamerejesha wananchi katika ratiba ya kawaida kufanya kazi.

Kwenye uchunguzi wa Taifa Leo, tangu tathmini ya saa kufanyika, katika maeneo ya Kasarani, Zimmerman, Githurai na Ruiru, wafanyabiashara hususan wa bidhaa za kula wanaendesha kazi zao hadi mwendo wa saa mbili na nusu au saa tatu kasorobo.

“Kati ya saa kumi na moja jioni hadi saa mbili, huo ndio muda wa wengi kutoka kazini. Ndio wakati ambao biashara katika masoko mengi huwa zimenoga. Tunahisi ni afueni kwetu,” John Njoroge muuzaji wa matunda katika soko la Jubilee, Githurai akasema.

Thika Road, kinyume na ilivyokuwa kabla ya mabadiliko ya saa ambapo magari yalikuwa machache, baada ya tangazo la Rais Kenyatta, shughuli za usafiri na uchukuzi kati ya saa moja za jioni hadi saa mbili na nusu zimeshika kasi.

Isitoshe, kati ya mtaa wa Githurai na Clayworks – Kasarani, mwendo wa jioni, watu wanaonekana wakitembea huru, taswira hiyo ikionyesha saa za awali za kafyu ziliwapimia uhuru wa kutembea na kutoka kazini.

Masharti na mikakati iliyowekwa imesifiwa na serikali kuwa imesaidia pakubwa kuzuia msambao wa ugonjwa wa Covid – 19, ambao umegeuka kuwa janga la kimataifa.

Rais Kenyatta amesema kufunguliwa kamilifu kwa uchumi kutategemea hali ya maambukizi, na tahadhari wanayochukua wananchi kuzuia msambao wa virusi vya corona.

Juni 6 katika hotuba yake kwa taifa, Rais alisema maandalizi ya kaunti kupambana na Covid – 19 pia yataamua iwapo uchumi utafunguliwa kufikia mwezi Julai au la. Alisema kila kaunti lazima iwe na kituo cha kulaza wagonjwa wa corona kisichopungua vitanda 300.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini, CoG, Bw Wycliffe Oparanya anasema ni kaunti 12 pekee kwa jumla ya 47 zilizoafikia matakwa hitajika.