• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Manchester City waruhusiwa kuandaa gozi dhidi ya Liverpool uwanjani Etihad

Manchester City waruhusiwa kuandaa gozi dhidi ya Liverpool uwanjani Etihad

Na CHRIS ADUNGO

MANCHESTER City wamepewa idhini ya kuandaa gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalowakutanisha na mabingwa wa msimu huu Liverpool mnamo Alhamisi ya Julai 2, 2020 uwanjani Etihad.

Awali, maafisa wa usalama walikuwa wamependekeza mechi hiyo kuchezewa katika uwanja mwingine tofauti nje ya jiji la Manchester ili kuepusha tukio la mashabiki kukongamana nje ya uwanja wa Etihad kinyume na masharti na hivyo kuibua makabiliano makali kati yao na polisi.

Maamuzi ya kuandaliwa kwa gozi hilo uwanjani Etihad hatimaye ni zao la kushauriana kwa maafisa wa usalama, maafisa wa afya, vinara wa vikosi husika na wasimamizi wa Baraza la Ushauri la Jiji la Manchester (SAG).

Liverpool walitwaa ufalme wa EPL msimu huu baada ya miaka 30 ya kusubiri kufuatia ushindi muhimu wa 2-1 uliosajiliwa na Chelsea dhidi ya Man-City mnamo Alhamisi ya Juni 25, 2020 uwanjani Stamford Bridge.

Ina maana kwamba Man-City watawaandalia Liverpool ya kocha Jurgen Klopp gwaride la heshima wakati wa mchuano huo ugani Etihad.

“Baada ya takriban mechi zote za hivi karibuni tangu kurejelewa kwa kipute cha EPL kuchezewa ndani ya viwanja vitupu, SAG imetoa idhini ya mchuano ujao kati ya Man-City na Liverpool kutandaziwa uwanjani Etihad kuanzia saa nne na robo usiku Alhamisi ya Julai 2, 2020,” akasema Diwani wa Luthfur Rahman ambaye ni mwanakamati mkuu wa Baraza la Jiji la Manchester anayehusika na masuala ya utamaduni na burudani.

“Sawa na mechi zote nyinginezo ambazo tumeshuhudia tangu Juni 17, 2020, mchuano kati ya Man-City na Liverpool utachezewa ndani ya uwanja mtupu bila ya mahudhurio ya mashabiki,” akaongeza.

Mashabiki wamezuiwa kuingia uwanjani kuhudhuria mechi za EPL au hata kukongamana nje ya viwanja kufuatilia michuano ya vikosi vyao kutokana na hofu ya kuenea zaidi kwa virusi vya homa kali ya corona japo soka ya Uingereza ilirejelewa rasmi mnamo Juni 17.

Kocha Jurgen Klopp alikuwa awali amepinga pendekezo la gozi hilo kuchezewa mbali na jiji la Manchester akisisitiza kwamba hatua hiyo ingewapa vikosi husika gharama isiyostahili ya usafiri, malaji na malazi.

Mechi nyinginezo ambazo maafisa wa usalama nchini Uingereza walikuwa wameomba vinara wa EPL kuziandaa katika viwanja visivyokuwa nyumbani kwa wenyeji ni gozi la Merseyside lililowakutanisha Everton na Liverpool mnamo Juni 21, 2020 na lile lililowakutanisha Manchester United na Sheffield United mnamo Juni 24, 2020.

Hata hivyo, mechi hizo ziliandaliwa hatimaye katika viwanja vya Goodison Park na Old Trafford mtawalia.

You can share this post!

Magoha ataka taasisi za kozi za ufundi zifunguliwe Septemba

Pedro Rodriguez kuagana na Chelsea na kujiunga na AS Roma

adminleo