Michezo

Reading anayochezea Mkenya Ayub Timbe yazimwa na Derby

June 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

WINGA matata Ayub Masika Timbe alionja mechi yake ya tatu kwenye Ligi ya Daraja la Pili Uingereza japo timu yake ya Reading ilisalimu amri kwa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Derby County uwanjani iPro, Jumamosi.

Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 27 alijaza nafasi ya Ovie Ejaria dakika ya 82.

Reading ya kocha Mark Bowen, ambayo haijafanikiwa kurejea Ligi Kuu tangu ishushwe mwisho wa msimu 2012-2013, ilifungwa mabao mawili ya haraka katika dakika mbili za mwisho za kipindi cha kwanza kupitia kwa Tom Lawrence na nahodha Wayne Rooney aliyefuma penalti iliyopatikana baada ya Martyn Waghorn kuangushwa ndani ya kisanduku.

Vijana wa Bowen walianza kipindi cha pili na ari kubwa ya kupata mabao. Walipoteza nafasi kadha kabla ya Sam Baldock kutikisa nyavu za Derby kupitia kichwa sekunde chache baada ya kujaza nafasi ya George Puscas dakika ya 61.

Licha ya Reading kutafuta mabao zaidi kwa bidii ya mchwa, haikufaulu na ikaishia kupoteza alama zote.

Timu zote mbili zimeshuhudia Matt Miazga (Reading) na Lawrence wakionyeshwa kadi nyekundu baada ya majibizano makali mara tu kipenga cha mwisho kilipolia.

Katika michuano mingine iliyokamilika kusakatwa Jumamosi kwenye ligi hiyo ya klabu 24, Preston ilizabwa 3-1 dhidi ya Cardiff City, Swansea ikalishwa 1-0 na Luton Town nayo Charlton ikazima Queens Park Rangers. Mechi kati ya Barnsley anayochezea Mkenya-Muingereza Clarke Oduor na Millwall ilitamatika 0-0.

Reading imesalia katikati mwa jedwali kwa alama 49 kutokana na mechi 39 nayo Barnsley bado inavuta mkia kwa alama 38 baada ya kusakata idadi sawa ya mechi.

Vikosi:

Reading (wachezaji 11 wa kwanza) – Rafael, Chris Gunter, Matt Miazga, Liam Moore (nahodha), Andy Rinomhota, John Swift, Ovie Ejaria, Yakou Meite, Michael Olise, Omar Richards, George Puscas; Wachezaji wa akiba – Sam Walker, Michael Morrison, Sam Baldock, Jordan Obita, Garath McCleary, Tyler Blackett, Ayub Masika, Charlie Adam, Pele. Derby County (wachezaji 11 wa kwanza) – Hamer, Wisdom, Forsyth, Waghorn, Lawrence, Clarke, Martin, Wayne Rooney (nahodha), Bogle, Sibley, Bird; Wachezaji wa akiba – Roos, Shinnie, Jozefzoon, Holmes, Lowe, Davies, Knight, Huddlestone, Whittaker.